Beki mpya Yanga ajipa majukumu mazito

Muktasari:

Beki huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumia klabu hiyo ya Jangwani akitokea Polisi Tanzania ambapo alitumikia timu hiyo msimu uliopita wa Ligi Kuu.

BEKI mpya wa Yanga, Yassin Mustapha ‘Evra’ amekiri kuwa ana jukumu zito la kuhakikisha anafanya vizuri na kuisaidia klabu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu kutwaa ubingwa.

Nyota huyo ametua Yanga akitokea Polisi Tanzania ambapo amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo.

Msimu uliopita Evra alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo ndani ya Polisi Tanzania ambapo alicheza mechi 34 za Ligi Kuu na kuwafanya maafande hao kumaliza ligi nafasi ya tano kwa pointi 55.

Beki huyo ambaye ana uwezo mkubwa kwenye kukaba na kufanya mashambulizi kabla ya kutua Polisi pia amepitia timu mbalimbali ikiwepo Polisi Dodoma, Stand United, Coastal Union na Mwadui FC.

Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Jumatatu Agosti 3, 2020, Evra amesema atahakikisha anapambana ili timu ifanye vizuri msimu ujao wa ligi.

Amesema kazi atakayoanza nayo ni kukomaa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kwa kuonyesha kiwango bora ambacho kitawavutia benchi la ufundi.

“Nimekuja hapa kwa lengo la kuipambania timu ndio maana wamenisajili hivyo ni lazima kwangu nipambane sana kuipa mafanikio klabu, nitakomaa kwa kila mchezo nitakaocheza.

"Najua pale nitakutana na changamoto ya namba hivyo nitakomaa kuwepo kikosi cha kwanza kwani sitakubali nikae benchi hivyo nitajituma kuanzia mazoezi hadi kwenye mechi ili kumridhisha kocha,” amesema Evra.