Beki Yanga achoshwa na Kagere

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa mchezaji mzawa kuchukua zawadi ya ufungaji bora Ligi Kuu ilikuwa ni msimu wa wa 2015/2016 ambapo ilichukuliwa na Saimon Msuva aliyekuwa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting


Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua amewataka washambuliaji, Reliants Lusajo, Paul Nonga na Yusuph Mhilu kuhakikisha nyota wa Simba, Meddie Kagere hachukui zawadi ya ufungaji bora msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Joshua alisema anaamini pindi ligi ikirejea, Lusajo wa Namungo na Mhilu wa Kagera Sugar wenye mabao 11 kila mmoja na Nonga wa Lipuli aliyepachika mabao 10, watakaza buti na kumpokonya tonge mdomoni Kagere ambaye kwa sasa anaongoza akiwa amepachika mabao 19.

"Alianza kuchukua Emmanuel Okwi kisha akachukua Kagere msimu uliopita,bado anaonekana ana mwelekeo wa kuchukua tena, wapo Lusajo,Mhilu na wengine ambao wanaweza wakapambana kuchukua kiatu,"

"Hao wazawa walikuwa kwenye moto wa kuotea mbali, naamini ligi ikianza watafanya vitu vikubwa,kinachotakiwa ni timu zao kuwapa ushirikiano,"amesema.

Mbali na wachezaji anaoamini watampindua Kagere,pia mtazamo wake ligi ikianza anaona itakuwa na ushindani utakaotokana na wanasoka kukumbuka kazi yao.

"Wachezaji wana hamu ya kufanya kazi, hivyo naamini watakuwa wanajituma kwa bidii ili kuonyesha ufundi wao,"amesema Joshua.