Beki Real Madrid anukia Inter Milan

Saturday June 27 2020
BEKI PIC

MILAN, ITALIA. INTER Milan inaripotiwa imekubali kulipa ada ya Euro 45 milioni,  kama ada ya usajili ili kumsajili beki wa pembeni wa  Real Madrid, Achraf Hakimi, anayecheza kwa mkopo Borussia Dortmund.
Taarifa hiyo kutoka Italia zinadai kuwa Inter wamefikia makubaliano na Real Madrid ili kuuziwa beki huyo ambaye ameonesha kiwango bora akiwa na klabu ya Dortmund aliyojiunga nayo kwa mkopo mwaka 2018.
Hakimi ambaye amekulia katika timu za vijana za Madrid kuanzia ile ya umri chini ya miaka 18, hadi kupandishwa timu ya wakubwa Julai, 2017, anatajwa kuwa atasaini mkataba wa miaka mitano na Inter Milan
Beki huyo anayeichezea timu ya Taifa ya Morocco ana umri wa miaka 22 ana uwezo wa  kucheza nafasi ya beki wa kulia na kushoto, kulingana na matakwa ya mwalimu husika na mahitaji ya mechi.
Ada ya usajili wake inatajwa kuwa ni Euro 40 milioni, lakini kutokana na bonasi inatazamiwa kupanda hadi kufikia Euro 45 milioni.
Mapema mwezi uliopita Madrid walitangaza kuwa wanahitaji kumrudisha ama kumpeleka sehemu nyingine kwa mkopo, lakini Hakimi mwenyewe alipinga jambo hilo na kuweka wazi kuwa ikiwa ataondoka Dortmund  basi aende kucheza timu itakayomsajili moja kwa moja, na sio kutolewa kwa mkopo.

Advertisement