Barbara: Simba subirini vitendo

Dar es Salaam. Ofisa mtendaji mkuu mpya wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez amesema kuwa yeye ni mtu wa kufanya kazi kwa vitendo na wala si maneno.

Barabara alisema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika wiki iliyopita.

Alisema kuwa yeye ni mtu mkali na anayejali muda katika kufanya kazi zake kwa wakati.

“Mimi ni mtu wa kufanya kazi kwa vitendo na wala sio kwa manenomaneno, nataka ufanisi zaidi na mpaka sasa najivunia kuwa mtu wa hivyo,” alisema Barbara.

“Niliwaambia wazazi wangu kuwa nataka kufanya kazi za kuitumikia jamii, nimepitia taasisi kadhaa mpaka kuwa mtendaji mkuu wa Klabu ya Simba, kote huko nimekuwa mtu wa vitendo.”

Alisema kuwa akiwa anafanya kazi katika Taasisi ya Mohammed Dewji (Mo Dewji Foundation), alikuwa na cheo cha mkuu wa wafanyakazi - kazi ambayo ilimfanya mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kumteua kuwa mmoja wa wakurugenzi wa klabu.

Alisema kuwa alifanya kazi hiyo kwa uadilifu na hata Senzo Mazingisa alipoondoka klabuni hapo, yeye aliteuliwa kuwa kaimu mtendaji mkuu.

“Sikupenda kuwa CEO (mtendaji mkuu), ilinichukua muda kuamua kukubali kwani nilikuwa na mipango mingine zaidi ya mpira,” alisema.

“Hata hivyo, wakurugenzi walinipigia kura na Mo kuniambia, ilinibidi kuacha mambo yangu mengine na kuingia katika cheo hiki cha sasa.”

Mwanamama huyo aliongeza kuwa, alipouliza kwa nini amepigiwa kura na wakurugenzi wote wa bodi ya klabu hiyo, jibu alilopata ni ufanisi wa kazi aliouonyesha katika kipindi cha takribani miaka minne.

Alisema kwa sasa anajisikia fahari kuiongoza klabu hiyo akiwa na umri mdogo huku akifichua namna alivyochangia kuajiriwa kwa Senzo katika klabu hiyo ambaye amehamia Yanga.

Barbara, mwenye umri wa miaka 30, alisema alikutana na Senzo nchini Afrika Kusini alipokwenda kumfanyia usaili wa ajira wakati klabu inatafuta mtendaji mkuu.

Alisema jukumu la kumfanyia usaili alipewa na bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo baada ya kuanzisha mfumo mpya wa uendeshaji.

Mtendaji huyo alisema kulikuwa na waombaji wengi katika nafasi hiyo, lakini baada ya kuuchambua uwezo wao waliona kuwa Senzo anazo sifa zote, lakini ili kujiridhisha ni lazima wamfanyie mahojiano ya ana kwa ana.

“Nilifunga safari na kwenda kukutana na Senzo, Afrika Kusini na kumfanyia mahojiano, nilifanya kazi hiyo kwa sababu nina uzoefu mkubwa kwani nimewahi kufanya kazi kampuni ya Deloitte.”

Alisema mbali ya kumfanyia usaili Senzo na baadaye kuanza kazi, bado yeye alifanya kazi nyingi za klabu na kuwaondoa wasiwasi wanachama na mashabiki kuhusiana na utendaji wake.

“Mimi nipo tofauti na vile watu wanadhani. Nataka zaidi kuona matunda na wala si maneno. Ni mkali kwenye kazi kwani nataka vitu vifanyike kwa ufanisi na si vinginevyo,” alisema Barbara.

Alisema kuwa Simba ni chapa kubwa kulinganisha na umri wake, lakini kutokana na uzoefu alioupata katika mashirika na taasisi mbalimbali alikofanya kazi ataleta ufanisi katika klabu hiyo.

“Mimi ni kiongozi, lazima niwe mbunifu katika kazi zangu na kuleta tija kwa klabu ya Simba, naomba niwatoe wasiwasi kuhusiana na hilo,” alisisitiza.

“Wanachama lazima wajue kuwa mimi sio kocha wala mchezaji, kazi yangu kubwa ni kuona kila idara inafanya kazi yake kwa mahitaji ambayo yataleta ufanisi mkubwa.”

Mtendaji huyo pia alisema huu ni wakati wa viongozi vijana kufanya kazi kubwa kwa ufanisi katika klabu na kuleta maendeleo makubwa ambayo yatawafanya kukumbukwa katika siku za usoni.

Changamoto

Akizungumzia njia bora ya kushinda changamoto zinazotokana na maneno ya watu, Barbara alisema ni kuziba masikio na kuendelea na majukumu kwa kuwa lengo kuu ni kuleta maendeleo.

Alisema akiwa kama binadamu kitendo cha kupongezwa au kusemwa vibaya ni jambo la kawaida kwani hata mtu akifanya mazuri mangapi sio kila mtu atamtaja kwa mazuri.

“Mimi ni Mtanzania ambaye ninaishi maisha ya kawaida sana. Kamwe sitaweza kukatishwa tamaa na maneno ya watu zaidi ya kuendelea na majukumu tu,” alisema.