Baba ampa sharti zito Tegete

Friday May 22 2020

 

By MASOUD MASASI,MWANZA

WAKATI Straika wa Alliance FC, Jerryson Tegete akirejea uwanjani baada ya  kukaa nje baada ya kupata jeraha la nyama ya paja,baba mzazi wa nyota huyo John Tegete amemtaka mwanaye kuhakikisha anafunga mabao sita (6) katika mechi tisa zilizobaki za ligi kuu.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga,Mwadui,Kagera Sugar alikuwa nje ya uwanja takribani miezi miwili akiuguza jeraha hilo ambapo hadi sasa ameshafunga mabao mawili ligi kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti,Tegete alisema walikubaliana na kijana wake kuwa  msimu huu wa ligi kuu  aweze kufunga angalau mabao kumi na kutoa pasi za bao zisizopungua 15.

Tegete alisema kabla ya kupata jeraha hilo Straika huyo tayari alishakuwa amefunga mabao mawili na kutoa pasi tano za mwisho zilizozaa bao kwenye kikosi chake cha Alliance.

Alisema jeraha hilo ndilo limemwaribia mwanaye kwani lilifanya akae nje ya uwanja akiuguza ambapo sasa amempunguzia idadi ya mabao kwa kumtaka afunge Nane pekee huku pasi za mabao zikipungua hadi 10.

“Unajua jeraha ndio limemuharibia kijana wangu tulikubaliana mambo mengi kabla ya ligi kuu kuanza lakini sasa amepona nimemwambia anifungie mabao sita tu na kutoa pasi za bao  tano kwenye mechi zilizobaki, ”alisema Tegete.

Advertisement

Alisema katika kipindi ambacho ligi ilisimama aliamua kumsimamia mazoezi yake ambapo alimfua vya kutosha hivyo sasa anaamini yuko fiti wala hana wasiwasi na idadi ya mabao aliyompa afunge.

“Tulikuwa na ratiba kwa siku anafanya mazoezi mara mbili niliamua kumsimamia mwanzo mwisho na nimeona yuko fiti kabisa kwani nilimkimbiza vya kutosha,” alisema Mzee huyo ambaye alishawahi kuwa kocha wa Toto Africans.

Advertisement