BADO! Alan Shearer anavyowatesa kina Mo Salah England

Tuesday May 19 2020

 

LONDON ENGLAND. MOHAMED Salah alivunja rekodi kibao katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Liverpool. Mastaa wengine kama Eden Hazard, Thierry Henry, Sadio Mane, Harry Kane kila mmoja na wakati wake alifanya kitu kilichoacha alama kwenye ligi hiyo, lakini wote hao wanateswa na mtu mmoja tu, Alan Shearer.

Kwa sasa, Shearer akiwa kwenye makochi akichambua soka, jina lake limebaki kwenye kumbukumbu za kudumu kwenye Ligi Kuu England kutokana na kuacha rekodi ambazo zimebaki kuwatesa tu kina Mo Salah, kwa sababu ni ngumu kinoma kuzivunja.

Kinara wa mabao wa muda wote

Wamepita mastaa wengi mahodari wa kufunga mabao kama Wayne Rooney, Ruud van Nistelrooy, Didier Drogba, Robbie Fowler, Thierry Henry, lakini wote hao wamechemsha kuvunja rekodi ya Shearer ya kufikisha mabao 260 kwenye Ligi Kuu England. Idadi hiyo ya mabao inamfanya Shearer kwa kinara wa kufunga wa muda wote kwenye Ligi Kuu England. Rooney alifurukuta kujaribu kuvunja rekodi hiyo, lakini amekomea kwenye mabao 194. Kwa maana hiyo, rekodi hiyo ya mabao itazidi kuwatesa mastaa wa Ligi Kuu England kwa sababu ni ngumu kuvunjika kirahisi.

Afunga mara nyingi hat trick

Shearer amefunga mabao 260 kwenye Ligi Kuu England. Kwenye mabao hayo, straika huyo wa zamani wa England ameweka rekodi ya kupiga tatu tatu kwenye mechi moja mara nyingi, akifanya hivyo mara 11. Hiyo ina maana, Shearer amefunga hat-trick nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye Ligi Kuu England.

Advertisement

Robbie Fowler anayemfuatia akiwa na hat-trick tisa na Henry na Michael Owen wamekomea kwenye hat-trick nane kila mmoja.

Wachezaji wengine wenye hat-trick nyingi kama Yakubu Aiyegbeni, Nicolas Anelka, Kevin Campbell, Les Ferdinand, Teddy Sheringham wamefanya hivyo wakiwa na zaidi ya timu tatu.

Kufunga mara nyingi msimu mmoja

Katika msimu wa 2017/18, Mo Salah alifunga mabao 32 kwenye Ligi Kuu England na kuwa mmoja wa mastaa waliofunga mara nyingi ndani ya msimu mmoja wa ligi hiyo. Kabla ya hapo, kulikuwa na wachezaji watatu tu waliokuwa wamewahi kufikisha walau mabao 31 kwenye ligi ndani ya msimu mmoja, Shearer akiwa Blackburn (1995-96), Cristiano Ronaldo akiwa Manchester United (2007/08) na Luis Suarez akiwa Liverpool (2013/14). Lakini, katika msimu wa zamani, Shearer bado anashika rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja wa ligi, alipofunga mara 34 katika mechi 42.

Kufunga penalti nyingi

Kwenye ile rekodi yake ya kufunga mabao 260 kwenye Ligi Kuu England yanayomfanya awe kinara wa mabao wa muda wote kwenye ligi hiyo, mabao mengine Shearer aliyapata kwa kupitia mikwaju ya penalti. Staa huyo ni mmoja wa wachezaji waliotumbukiza mipira mingi kwenye nyavu kwa kupitia penalti, ambapo amefunga mabao 56 kwa staili hiyo na hivyo kuwa mchezaji aliyefunga mara nyingi kwa mikwaju hiyo. Kama ilivyo kwenye rekodi ya kufunga, Shearer amekosa mara nyingi pia mikwaju yake ya penalti, akifanya hivyo mara 11.

Mfungaji mdogo wa hat trick

Kabla ya kwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 1995/96 akiwa na kikosi cha Blackburn Rovers na kisha kuwatesa mabeki wa timu pinzani alipo- kuwa kwenye chama la Newcastle United, Shearer alianzia kuonyesha cheche zake ndani ya uwanja tangu akiwa Southampton, alikoibukia. Akiwa kwenye kikosi hicho cha wakali wenye maskani yao St Mary’s, Shearer aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuwahi kufunga hat trick kwenye Ligi Kuu England. Staa huyo alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Arsenal, mwaka 1988 ambapo Shearer wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17 na siku 240. Southampton iliichapa Arsenal, 4-2.

Mfungaji bora wa Desemba

Usishangae. Huo ndio ukweli, kwenye miezi yote iliyoshuhudia Ligi Kuu England ikipigwa, Desemba ulishuhudia staa Shearer akifunga mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yeyote kuwahi kufanya hivyo. Wakati makocha wengi kwenye ligi hiyo pamoja na wachezaji wakiamini kwamba Desemba ni kipindi kigumu kutokana na ligi kushuhudia mechi nyingi zikichezwa huku kukiwa na hali ya baridi kali huko Ulaya, lakini kwa Shearer alichukua hiyo kama fursa ya kufunga mabao mengi zaidi.

Ndani ya mwezi Desemba, Shearer amefunga mabao 39 na kuwa mchezaji aliyefunga mara nyingi kuliko yeyote. Mchezaji anayemfuatia ni Rooney, ambaye amekomea kufunga mara 31.

Mfungaji bora Newcastle

Kila mtu ana eneo lake analoweza kuweka rekodi. Rooney ni kinara wa mabao wa muda wote huko Man United, Henry huko Arsenal na Frank Lampard kwenye kikosi cha Chelsea. Lakini, Shearer anawapa wakati mgumu wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Newcastle United katika kufukuzia kuvunja rekodi yake ya kuwa mfungaji wa mabao mengi zaidi katika kikosi hicho cha St James’ Park. Shearer hadi anastaafu kwenye kikosi hicho alikuwa amefunga mabao 148 na kuwaacha mbali sana waliokuwa wakimfuatia kama Peter Beardsley, Shola Ameobi na Les Ferdinand.

Kuhusu rekodi ya uhamisho duniani

Harry Maguire wakati ananaswa na Man United mwaka jana kwa ada ya Pauni 85 milioni, ilimfanya avunje rekodi ya kuwa beki ghali zaidi duniani.

Lakini, rekodi ya jumla ya mchezaji ghali ilibaki kuwa chini ya Neymar. Basi kwa wachezaji wa England, hadi sasa hakuna aliyevunja rekodi ya Shearer ya kuwa mchezaji ghali aliyevunja rekodi ya uhamisho duniani. Julai 1996, wakati Newcastle ilipomsajili Shearer, ililipa Pauni 15 milioni, pesa ambayo iliweka rekodi ya dunia kwa wakati huo kwenye uhamisho. Tangu hapo, wachezaji wengi wa England wamesajiliwa kwa pesa nyingi kuliko dau hilo, lakini hakuna aliyeweza kuvunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho. Taji hilo bado linashikiliwa na Shearer.

Advertisement