Azam FC yawasogeza mashabiki karibu

Muktasari:

Azam yawasogeza karibu mashabiki zao wa Temeke.

KLABU ya Azam FC imeamua kutengeneza upya mtaji wa mashabiki wake baada ya kuanzisha tamasha lao (Azam Festival) litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu likiwakutanisha mashabiki wa soka kutoka vitongoji vyote vya Temeke.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Agosti 14, 2020, Afisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zakaria amesema tamasha hilo litajumuisha timu kutoka Wilaya ya Temeke kwani ndio watu wao wanaowazunguka.

"Kutakuwa na mechi lakini zitawahusisha watu wa Chamazi sana, zipo timu ambazo zitaalikwa, siku ya kwanza kutakuwa na matukio tofauti, kutakuwa na Jogging za Chamazi na wamealika watu wengine".

"Tutakuwa na mgeni rasmi, tumealika vyombo vya habari kwa ajili ya kuja kucheza mechi za mpira wa miguu kwa wale wenye timu za mpira na kila mwaka tutakuwa tunashirikiana nao,".

Zaka amesema uzinduzi utaanza Agosti 16 lakini kuanzia Agosti 17 mwaka huu ndio mechi zitaanza kuchezwa katika viwanja mbalimbali na Agosti 23 nusu fainali itachezwa Uwanja wa Azam Complex.

"Viwanja vitakavyotumika ni shule ya msingi Chamazi, uwanja wa Songasi na hizi mechi zitachezwa huko mpaka hatua ya robo fainali, wakati nusu na fainali yenyewe basi zitachezwa Uwanja wa Azam Complex,".

Aliongeza kwa kusema baada ya fainali kutakuwa na mechi kutoka timu za vijana, baada ya hapo watacheza timu kubwa na timu nyingine ambayo zimealikwa na wataitangaza.

"Zawadi kila timu iliyoingia fainali atapewa jezi, kuna vikombe na pesa taslimu ambayo bado tunaijadili, timu zote viingilio ni bure kwa sababu ni mashabiki wetu,".