Aucho apata dili la maana Misr El-Makkasa

Muktasari:

  • Kabla ya kwenda India, Aucho alizichezea, Simba ya Uganda, Tusker na Gor Mahia za Kenya, Baroka ya Afrika Kusini na Red Star Belgrade, OFK Beograd za Serbia.

Dar es Salaam. Kiungo wa kimataifa wa Uganda, Khalid Aucho amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Misr El-Makkasa inayoshiriki Ligi Kuu Misri.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa sehemu ya timu ya taifa ya Uganda iliyoishia katika hatua ya 16 bora ya fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri.

Kiwango alichokionyesha Aucho ndicho kilichoivutia  Misr El-Makkasa, ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya  sita katika msimamo wa Ligi Kuu Misri.

Aucho amekuwa mchezaji wa pili kusajiliwa kipindi hiki cha usajili wa kwanza ni Salah Amin kutoka Nogoom FC, mkataba wake umegharimu, Dola 600,000.

Mganda huyo amejiunga na El-Makkasa akitokea India alipokuwa akiichezea Churchill Brothers yenyewe alijiunga nayo, Julai mwaka jana.

Misr El-Makkasa wanatakiwa kumuuza miongoni mwa wachezaji wake wa kigeni ambao ni John Antwi, Kevin Muhire, Shimelis Bekele au Paulin Voavy ili kumpisha Aucho.