Atabaki,habaki Liverpool kutumia pesa kumtuliza Van Dijk

Muktasari:

Beki wa Paris Saint-Germain, Thiago Silva, 35, analipwa Pauni 300,000 kila baada ya siku saba, akiwa beki mwingine anayelipwa mshahara mkubwa kuliko ambao atalipwa Van Dijk huko Anfield atakapokamilisha kusaini dili jipya.

LIVERPOOL, ENGLAND. LIVERPOOL wanapoamua kujidanganya kuhusu Virgil van Dijk. Wanajua wazi kwamba beki huyo wa kati iliyemsajili kwa mkwanja mrefu, Pauni 75 milioni anawindwa na timu zinazojua kugawa mishahara mikubwa kwa mastaa wake.

Sasa kusikia hivyo na wao wameamua kuandaa Pauni 50 milioni kumpa Van Dijk kumpandishia mshahara wake ili kuzikata maini timu zinazomdanya Mdachi huyo kama vile Juventus.

Van Dijk, 28, ameandaliwa mkataba wa miaka mitano ili kubaki kwenye kikosi hicho cha Anfield kwa muda mrefu kukitumikia kikosi cha Mjerumani Jurgen Klopp. Dili hilo jipya litamshuhudia beki huyo akilipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki ikiwamo bonasi ikiwa ni ongezeko la Pauni 75,000 katika mshahara wake wa wiki kwa huu anaolipwa kwa sasa.

Lakini, Liverpool kama inadhani kumpa Van Dijk, Pauni 200,000 kwa wiki kutamtuliza asiondoke inajidanganya, huko kwenye klabu nyingine ikiwamo Juventus kuna mabeki wa kati wanaolipwa mishahara mikubwa kwelikweli.

Ukiwachukulia Juve tu, ambao wameripotiwa kutenga Pauni 150 milioni ili kumng’oa Van Dijk kutoka Anfield, wenyewe wanamlipa beki wao wa kati, Mdachi mwingine, Matthijs De Ligt, 20, Pauni 416,000 kwa wiki.

Hiyo ni zaidi ya Pauni 116,000 kwa wiki, tofauti ya De Ligt na Van Dijk kwenye mshahara, huku ikidaiwa kwamba bila ya shaka kama VVD aking’oka Anfield na kwenda Turin, atakwenda kulipwa kibosi zaidi na pengine atakuwa beki anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.

Beki wa Paris Saint-Germain, Thiago Silva, 35, analipwa Pauni 300,000 kila baada ya siku saba, akiwa beki mwingine anayelipwa mshahara mkubwa kuliko ambao atalipwa Van Dijk huko Anfield atakapokamilisha kusaini dili jipya.

Mabeki wa kati wengine wanaolipwa mshahara kuliko hata dili atakalopewa Van Dijk ni Lucas Hernandez, 23, anayelipwa Pauni 250,000 kwa wiki huko Bayern Munich, Gerard Pique wa Barcelona, anayelipwa Pauni 220,000 kwa wiki, Marquinhos wa PSG, anayelipwa Pauni 216,000 kwa wiki na Samuel Umtiti, anayepokea Pauni 210,000 kwa wiki kwa huduma yake anayotoa huko Nou Camp.

Kwenye dili hilo ambalo ataingia Van Dijk likifanikiwa basi, ataungana na mabeki wengine wa kati wanaolipwa Pauni 200,000 kwa wiki, akiwamo Sergio Ramos na Marcelo, wote kutoka Real Madrid ambapo wanalipwa mkwanja huo kwa huduma zao za kila wiki.

Beki ghali zaidi kwa sasa, Harry Maguire, aliyesajiliwa kutoka Leicester City kwa Pauni 85 milioni kwenda kukipiga Manchester United, analipwa mshahara wa Pauni 190,000 kwa wiki.

Hata hivyo, kitu ambacho kitamfariji Van Dijk ni kwamba kama atasaini dili lake jipya basi atakuwa beki anayelipwa mkwanja mrefu zaidi kwenye Ligi Kuu England. Rekodi yake ya kuwa beki ghali ilivunjwa na Maguire, lakini sasa atatamba tena kwenye mshahara ambapo hapo, atakuwa amemzidi mpinzani wake huyo kwa tofauti ya Pauni 10,000 kwa wiki.

Jambo hilo bado haliiafanyi Liverpool kuwa kwenye mikono salama kutokana na SunSport kusisitiza kwamba Juventus imeendelea kushikilia msimamo wake wa kutenga pesa za kumsajili Mdachi huyo.

Juventus inahitaji taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na inaamini kwa kuwa na Cristiano Ronaldo kwenye safu yake ya ushambuliaji ambaye ilimng’oa kutoka Real Madrid, haitakuwa shida kutimiza ndoto yao itakapomnasa beki, Van Dijk kutoka Liverpool kukipiga kwenye beki yao.