Arsenal yamfuta kazi Unai Emery

Muktasari:

Na sasa kikosi hicho cha Emirates kitakuwa chini ya Freddie Ljungberg kwa kipindi cha mpito. Arsenal wamesema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kutofurahishwa na matokeo ya uwanjanni na kiwango cha timu kwamba haichezi kwenye ubora unaotakiwa.

LONDON, ENGLAND . KOCHA, Unai Emery amefutwa kazi na Arsenal baada ya kuinoa timu hiyo kwenye miezi 18 tu.
Mhispaniola huyo,ambaye aliongoza Paris Saint-Germain kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ufaransa na kushinda mataji matatu ya Europa Leagues akiwa na Sevilla, aliteuliwa kuwa kocha wa Arsenal Mei 2018, alipotua Emirates kurithi mikoba ya Arsene Wenger.
Na sasa kikosi hicho cha Emirates kitakuwa chini ya Freddie Ljungberg kwa kipindi cha mpito. Arsenal wamesema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kutofurahishwa na matokeo ya uwanjanni na kiwango cha timu kwamba haichezi kwenye ubora unaotakiwa.
Arsenal imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi saba mfululizo na kipigo cha mabao 2-1 nyumbani uwanjani Emirates kutoka kwa Eintracht Frankfurt kwenye Europa League Alhamisi ndicho kilichofikisha mwisho ajira ya Mhispaniola huyo.
Arsenal haijashinda kwenye Ligi Kuu England tangu Oktoba 6 na sasa wapo nyuma kwa pointi nane kuifikia Top Four, ambayo ndio msingi mkuu wa timu hiyo kwa msimu huu katika kuifukuzia nafasi ya kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosa kwa misimu kadhaa.
Ljungberg alianza kuisimamia timu hiyo kwenye mazoezi ya Ijumaa na taarifa ya Arsenal ilisomeka: "Tuna umani kubwa na Freddie kwamba atatupeleka mbele.
"Msako wa kocha mpya unaendelea na tutatangaza rasmi jambo hilo litakapokamilika."
Kwa wiki nzima kumekuwa na maelezo kwamba Arsenal inamfikiria kocha wa Wolves, Nuno Espirito Santo kwenda kuchukua mikoba hiyo ya Emery, huku makocha wengine wanaopewa nafasi ni Mauricio Pochettino, Mikel Arteta, Massimiliano Allegri na Eddie Howe wa Bournemouth.