Alliance yaibomoa Biashara United

Friday July 12 2019

 

By Saddam Sadick

MWANZA.ALLIANCE FC inaendelea kujiimarisha kwa msimu ujao wa Ligi Kuu baada ya kumnasa straika wa Biashara United, Dany Manyenye.

Ujio wa straika huyo aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja unafikisha nyota wanne wapya waliotua klabuni hapo.

Waliosaini awali ni mabeki, Erick Murilo na Amimu Abdul pamoja na kiungo, Hussein Kassanga wote kutoka Mbao FC ambako walimaliza mikataba yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Alliance, Yusuph Budodi alithibitisha kumsainisha nyota huyo huku akitamba msimu ujao watatisha.

Alisema usajili wa mchezaji huyo ni mwendelezo wa kukisuka kikosi chao ili wanafanye vizuri na kushika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Usajili unaendelea na siku chache mbeleni tutakuwa tumekamilisha rasmi kikosi kitakachotumika msimu ujao, uongozi umejipanga na malengo ni kufanya vizuri,” alisema Budodi.

Alisema wanasubiri kuwasili kwa kocha wao, Malale Hamsini ili waanze maandalizi ya msimu mpya na wanahitaji kuingia kambini mapema.

“Kuhusu kocha tutaendelea na Malale licha ya kwamba alikuwa na ofa nyingine, lakini amekubali kurudi Alliance, hivyo tunasubiri aje atupe ratiba zake za maandalizi,” alisema.

Advertisement