Allegri tayari ana dili England

Saturday February 15 2020

Allegri tayari ana dili England,KOCHA, Max Allegri ,Manchester United,Ligi Kuu England,Top Four,

 

MILAN, ITALIA. KOCHA, Max Allegri ana bonge la dili mezani kwake la kwenda kuinoa moja ya klabu kubwa kwenye Ligi Kuu England kwa mujibu wa taarifa za kutoka Italia, huku ikikumbukwa kwamba bosi huyo wa zamani wa Juventus huko nyuma alihusishwa na Manchester United.
Allegri ameachana na Juventus tangu mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuwapa wababe hao wa Turin mataji matatu mfululizo kwenye Serie A. Lakini, kumekuwa na uvumi kwamba Juve wanamtaka tena baada ya mambo kuwa mazito sana kwa mrithi wake, Maurizio Sarri.
AC Milan nao wanahusishwa na mpango wa kumchukua Allegri, lakini Corriere dello Sport linaripoti kwamba Allegri, 52, tayari ana dili lake la kwenda England. Bado haifahamiki ni klabu gani ya England atakayokwenda licha ya kuhusishwa sana na Man United siku za nyuma. Man United kwa sasa ipo chini ya Ole Gunnar Solskjaer, ambaye atapewa muda wa kujaribu kuweka mambo sawa.
Man United kwa sasa ipo pointi sita nyuma ya kuifikia Top Four, nafasi inayotoa fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kama timu itashindwa kufanya hivyo msimu huu, basi Solskjaer atafunguliwa mlango wa kutokea.
Lakini, timu nyingine inayodaiwa kwamba Allegri anaweza kwenda kuchukua kazi ni Manchester City, ambako kumekuwa na mashaka makubwa juu ya majariwa ya Pep Guardiola kama atabaki kwenye timu huku akisakwa na Juventus. Allegri alihusishwa pia kwenda Arsenal kabla ya Unai Emery kufutwa kazi mwishoni mwa mwaka jana, lakini miamba hiyo ya Emirates iliamua kumpa kazi mchezaji wao wa zamani, Mikel Arteta. Dili nyingine ambazo zilihusisha jina lake kutajwa ni huko Chelsea, ambako walimchukua Frank Lampard na Tottenham Hotspur, walikomchukua Jose Mourinho baada ya kumwondoa Mauricio Pochettino.

Advertisement