Afrika Mashariki tusijifariji kufungwa na Senegal, Algeria

Muktasari:

Mwaka wa 2002, Senegal ilishindwa kubeba taji hilo dhidi ya Cameroon katika fainali mashindano ambayo yaliandaliwa nchini Mali.

HAUCHI hauchi hatimaye umekucha. Kila killicho na mwanzo hakika hakikosi mwisho.

Mashindano ya kuwania ubingwa wa Mataifa barani Afrika (AFCON) yanafikia kikomo mwishoni mwa wiki baada ya wababe miwili kupatikana.

Kama unakumbuka timu zilikuwa 24, lakini kufikia sasa ni miamba miwili ya soka barani Afrika imepata nafasi ya kunyaka taji katika mashindano hayo.

Mbivu na mbichi zitajulikana Ijumaa wakati Senegal na Algeria zitakapokutana katika fainali hizo ambayo inaandaliwa katika nchi ya Pharaohs jijini Cairo, Misri ama kwa wanaopenda Lugha ya Kimombo huita Egypty.

Senegali ikiongozwa na kocha mzawa Aliou Cisse ambaye alikuwa nahodha wa taifa hilo enzi zake wakati akicheza soka, ameingia fainali hizo kwa mara ya kwanza kama kocha na kwa Senegali ni mara yake ya pili.

Mwaka wa 2002, Senegal ilishindwa kubeba taji hilo dhidi ya Cameroon katika fainali mashindano ambayo yaliandaliwa nchini Mali.

Cameroon ikishinda kupitia mikwaju ya penalti 3-2 baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 0-0.

Katika penalti hizo, Aliou Cisse alikosa mojawapo.

Kwa hivyo Senegali kikosi ambacho kinaongozwa na mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane ipo ndani ya fainali hizo na ina kila sababu ya kuweza kunyakua taji hili.

Safari yake ilianza na kuinyuka Tanzania mabao 2-0, ikapoteza 1-0 dhidi ya Algeria na kuinyuka Harambee Stars Kenya 3-0.

Hayo yalifanyika katika makundi. Katika 16-Bora iliiondoa Uganda kwa bao 1-0. Robo fainali ikailaza Benin bao 1-0. Ikaingia nusu fainali ilikoilaza Tunisia 1-0 na kutinga fainali.

Shughuli ipo siku ya Ijumaa. Inakutana fainali na Algeria ilioishinda 1-0 ilipokutana nayo mapema katika awamu ya makundi.

Algeria imelishinda taji hili mara moja tu mwaka 1990 wakati ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Kazi ipo kwa Kocha Djamel Belmadi kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza lakini kwa nchi itakuwa mara ya pili.

Tangu mechi hizo zianze kwa kweli Algeria imenwafurahisha watu wengi sana kwa vile wanavyopiga soka lao kwa njia ya ustadi na ya kuelewana.

Ushindi wake wa juzi Jumapili usiku dhidi ya Nigeria haukuwa wa kubahatisha.

Ikiwa na wachezaji hodari kama mshambuliaji wa Manchester City, Riyad Mahrez, kuna kazi ya kufanya kwa ngome ya Senegal ambao itamkosa beki wake, Kalidou Koulibaly katika mechi hiyo ya fainali akitumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Algeria pia ilikuwa kwenye Kundi la C na timu za Taifa Stars na Harambee Stasrs.

Safari yake hadi kufikia hatua ya fainali iliinyuka Harembee mabao 2-0, Senegal 1-0 na Taifa Stars mabao 3-0.

Baada ya kuingia hatua ya 16 Bora ikainyuka Guinea mabao 3-0.

Ikaiondoa Ivory Coast kwa njia ya penalti baada ya mechi kuishia 1-1 katika dakika 120.

Nusu fainali ikainyorosha mabingwa wa filamu za kizushi Nigeria 2-1, Riyad Mahrez akipiga shughuli zake za kama kawaida katika dakika za mwisho za mchezo huo. Bonge la hikabu.

Fainali ndio hii hapa siku ya Ijumaa. Itakuwa ni Man City ama Liverpool? Yaaani ni Mahrez ama Sadio Mane? Mastaa hao wameshatoa ubabe wao Uingereza na kuuleta AFCON.

Sisi ni kuweka macho tu. Ni timu ambazo zilikuwa katika kundi moja. Kundi ambalo lilijumuisha Tanzania na Kenya.

Sijui Mwana Afrika Mashariki mwenzangu unajisikiaje kwa timu hizo kufikia hatua hiyo. Kumbuka Senegal na Algeria zimepita kwenye migongo yetu kufikia hatua hii.

Hapa nadhani tunajua sasa tulikuwa na tunakutana na timu za aina gani katika kundi letu.

Timu hizo zilikuwa na viwango bora sana kuliko timu zetu za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zote zimefungwa na Segenal kwa nyakati tofauti.

Uganda alifungwa katika hatua ya 16 Bora na hizo nyingine kwenye hatua ya makundi.

Kilichopo sasa, tuangalie mfumo wa hizi timu na kuweza kujifunza pale ambapo tuliangukia. Inatubidi kujua kuwa wenzetu waliwekeza na kuvitunza vipaji vya vijana wao na kuweza kuwa na timu imara kama hizi ambazo tumeziona kwa kucheza nazo.

Leo timu hizo zimefika fainali. Tusifarijike na kusema kuwa tumefungwa na timu kali tu. Bali tuboreshe viwango vyetu.

Kama si hivyo, tutaishia kutazama kwenye runinga kila mwaka na kuchagua timu za wenzetu kuzishangilia. Binafsi naipata Algeria nafasi ya kunyakua taji hilo. Soka ambalo inapiga inastahili kunyakua taji hilo. Ni siku tu. Siku hiyo ni Ijumaa. Saa nne usiku. Usikae mbali. Cheza karibu na runinga yako. Lazima kieleweke Ijumaa hii.