Adolph aanika kilichomuangusha Simba

Friday November 8 2019

Adolph -aanika- kilichomuangusha- Simba-Tanzania Prisons-Mohamed-Rishard-Adolph-kocha-Aussems-Michezo blog-Mwanasport-MwanaspotiSoka-

 

By Mwandishi Wetu

PRISONS mpaka sasa ndio timu pekee ambayo haijaonja kipigo katika Ligi Kuu Bara na jana iliwakomalia vinara, Simba na kutoka nao suluhu jijini Dar es Salaam, lakini kocha wake, Mohammed Rishard 'Adolph' ametaja tatizo linalomuangusha kwenye mechi zao ikiwemo wa jana.
Rishard alisema vijana wake wana tatizo kubwa la umaliziaji, hivyo wanatakiwa kulifanyia kazi jambo hilo ili waweze kupata ushindi katika michezo inayofuata.
Prisons awali ilikuwa na tatizo kubwa la katika eneo la ulinzi baada ya michezo mitatu mfululizo kutangulia kufunga bao na kisha mabao hayo kurudi.
Katika mchezo dhidi ya Kagera uliofanyika Oktoba 19 ilianza kufunga bao dakika ya 5 kupitia kwa Ismail Aziz kabla ya Kagera Sugar kusawazisha dakika ya 78.
Pia Oktoba 31 katika mchezo dhidi ya Alliance ilianza  kufunga kupitia kwa Samson Mbangula kabla ya Alliance kusawazisha dakika za mwisho kwa penalti.
Pia timu hiyo  imekuwa na shida hata katika umaliziaji kwani katika michezo 10 iliyocheza ukiwemo wa jana dhidi ya Simba imetoka sare michezo saba na kushinda mitatu huku ikifunga mabao 10.
Prisons imeshinda michezo mitatu tu kati ya 10 iliyocheza mpaka sasa kwani  imezifunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0,Mtibwa Sugar mabao 3-1, na JKT kwa bao 1-0  huku ikitoka sare ya 2-2 na Lipuli, 1-1 na Mbao, Alliance Fc na Kagera Sugar na ikatoka suluhu na Mbeya City,  Biashara United na Simba.
Kocha Rishard amesema eneo la ulinzi kwa sasa limetulia lakini bado kuna tatizo la umaliziaji linawafanya wakakosa sana mabao licha ya kutengeneza nafasi za kufunga.
"Ukiangalia katika mchezo dhidi ya Simba licha ya kwamba wapinzani wetu walitupa wakati mgumu, lakini tulijaribu kutengeneza nafasi kadhaa kwa  mipira ya kushtukiza lakini  umalizaji mbovu ukatunyima pointi tatu."
"Kama tungekuwa tuko vizuri katika umaliziaji wa nafasi tulizopata basi tungemaliza mchezo huo kwa ushindi.
"Tunaendelea kulifanyia kazi eneo hilo na naamini vijana wangu ni waelewa na watafanya vizuri zaidi katika michezo itakayofuata," alisema Rishard.

Advertisement