Adam Adam afunga hat trick ya kwanza VPL

Sunday October 25 2020
adamu pic

NYOTA wa JKT Tanzania, Adam Adam amefunga hat trick ya kwanza katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2020/21 huku akiiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga.

Katika mchezo huo ambao JKT Tanzania walikuwa ugenini, Adam alifungua akaunti yake ya mabao dakika ya 24 kabla ya Daniel Lyanga kupiga msumari wa pili na kwenda mapumziko wakiwa mbele.

Hadi dakika ya 52, Mwadui walijikuta wakiruhusu mabao mengine mawili huku wafungaji wakiwa wale wale Adam na mwenzake Lyanga na kuwafanya wenyeji hao kuwa na mlima mrefu wa kupanda.

Dakika ya 62, Mwadui walipata bao kupitia kwa nyota wa zamani wa Simba na Mbao FC, Pastory Athanas.

Bao hilo ambalo walipata Mwadui ni kama liliwachochea kasi JKT Tanzania ya kuendelea kutafuta mabao mengine, yule yule aliyepachika bao la kwanza kwenye mchezo huo, Adam alikamilisha hat trick yake kwa kupachika bao lake la tatu  dakika ya 82.

Ukuta wa Mwadui ni wazi ulizidiwa nguvu na safu ya ushambuliaji ya JKT Tanzania na kujikuta ikiruhusu bao la sita ambalo safari hiyo walifungwa na Said Luyaya ndani ya muda wa nyongeza (90+2).

Mchezo wa Mwadui dhidi ya JKT Tanzania ndio mchezo ambao hadi sasa umezaa mabao mengi zaidi (7) Ligi Kuu Bara, awali mchezo kati ya Azam dhidi ya Kagera Sugar  (6) ndio uliokuwa ukiongoza na Mwadui imekuwa timu ya kwanza kupata ushindi wa mabao mengi katika mechi moja.

Advertisement