Kocha Stars awapika wachezaji wake kisayansi

Muktasari:

Vifaa hivyo kwa hapa nchini vilianza kutumika katika klabu ya Azam Fc na baadaye Yanga  kisha Simba na sasa ni zamu ya Taifa Stars.

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa Tanzania 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije amewapima nyota wake uwezo wa kukimbia kwa kutumia vifaa maalumu wanavyotakiwa kuvaa ili kuonyesha mikimbio ya kila mmoja awapo uwanjani

Stars imeanza mazoezi yake leo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi utakaofanyika Jumapili kwenye uwanja huo.

Katika mazoezi hayo wachezaji wote wanaocheza nafasi za ndani walitakiwa kuvua jezi zao za juu kisha walivalisha vifaa hivyo.

Kwa upande wa wa makipa, Aishi Manula, David Kissu na Metacha Mnata, wao walitakiwa kuvaa juu ya jezi zao ikiwa ni tofauti na wachezaji wengine.

Baada ya kuvaa vifaa hivyo wachezaji walitakiwa kupasha misuli kwa kuchezea mipira kidogo na kupigiana pasi wao kwa wao.

Baada ya zoezi hilo, walihamia kwenye mazoezi ya kupita katika koni kwa takribani dakika 25.

Baada ya mazoezi hayo, kocha msaidizi, Seleman Matola aliwapumzisha wachezaji wake kwa kunyoosha viungo, kisha aliwapanga kwa makundi ya wachezaji sita na kuwataka wacheze kwa kugusa mpira mara mbili tu (Two Touch).

Wachezaji waliokuwepo katika mazoezi hayo ni Metacha Mnata, Aishi Manula, David Kissu, Shomari Kapombe, Israel Patrick, Mohamed Hussein, David Bryson, Abdallah Kheri, Idd Mobby, Jonas Mkude, Idd Seleman, Salum Abubakari, Said Ndemla, Ditram Nchimbi, Feisal Salum, Dickson Job, Mzamiru Yassin, Bakari Mwamnyeto na Ally Msengi.