Yanga hiyoo kileleni

Muktasari:

Yanga itashuka tena dimbani Septemba 27 kuikabili Mtibwa Sugar ugenini kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Yanga imeifunga Kagera Sugar bao 1-0 na kupanda kileleni kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kufikisha pointi saba.
Timu hiyo imeishusha KMC yenye pointi sita na ambayo ina mechi Jumatatu dhidi ya Mwadui ugenini huku pia ikiishusha Azam yenye pointi sita pia ambayo inacheza kesho na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Mukoko Tonombe ndiye aliyepeleka kilio Kagera Sugar baada ya kufunga bao dakika ya 71 akimalizia pasi ya Tuisila Kisinda.
Baada ya kufunga bao hilo Mukoko alikimbia hadi kwenye kibendera cha kona na kuwaita wenzake na kuwaambia wakae chini kisha kuonekana kama anawafundisha hivi hivyo kuamsha shangwe kwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo kwenye uwanja wa Kaitaba ambao muda mwingi walikuwa kimya.
Hata hivyo Yanga licha ya kushinda mchezo huo na kumiliki mpira lakini ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi za kupata bao jambo ambalo hata kocha wa kikosi hicho,Zlatko Krmpotic  amekiri.
Zlatko amewapa hongera wachezaji wake kwa ushindi licha ya kukiri mchezo ulikuwa mgumu kwani Kagera Sugar ni timu nzuri.
"Tulitengeneza nafasi mbili tatu na kuweza kutumia moja hivyo nawapa hongera timu yangu kwa ushindi ingawa nahitaji kuona tukicheza vizuri zaidi katika michezo ijayo", amesema Zlatko.
Kocha wa Kagera Sugar,Mecky Maxime amesema wameumia kwani walicheza vizuri lakini wapinzani wao walitumia nafasi moja na kuitumia kuwafunga bao.
"Mechi ilikuwa nzuri na tulikuwa na matarajio ya kushinda ili kurejesha morali katika kikosi changu baada ya kutopata matokeo mazuri michezo miwili iliyopita, lakini bahati mbaya tumepoteza na huu hivyo lazima tujipe pole wote.Bado kuna michezo mingine bele naamini tutapata ushindi", amesema Maxime.