Straika Namungo aipania Simba

Muktasari:

Fainali ya ASFC imetabiriwa kuwa ngumu kutokana na malengo ya timu hizo, kama anavyosema Reliants Lusajo wa Namungo FC kwamba wanataka kuweka rekodi, pia wanaamini Simba nao wanataka rekodi yao.

STRAIKA wa Namungo FC, Reliants Lusajo ameizungumzia fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), wanayocheza na Simba kesho Jumapili kwamba itakuwa ngumu kutokana na rekodi wanazotaka kuziweka.

Lusajo amesema kila timu inahitaji kuchukua taji la ASFC, kitu ambacho ameona haitakuwa mechi rahisi, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanatimiza ndoto hiyo.

Amesema lengo  ilikuwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania (VPL),ambayo wamemaliza wakiwa nafasi ya nne, na pointi 64, wakiwa wameshinda mechi 17, sare 13,walifungwa nne katika michezo 38 waliyocheza na baada ya kukosa taji la Ligi Kuu wanaelekeza nguvu ASFC.

"Fainali hii haitakuwa rahisi kama mashabiki wanavyoitabiri kuona hatuna chakupoteza, tunataka heshima ya kuchukua kombe na kuvaa medali, angalau Simba wao wamevaa ya VPL.

Ni fahari ya mchezaji kupata kifuta jasho cha msimu baada ya kufanya kazi ngumu, tukivaa medali ya ubingwa wa ASFC kwetu itakuwa faraja kubwa na kuweka alama ya kukumbukwa ama kuja kuvunjwa na timu nyingine msimu ujao,"amesema.

 

Namungo FC wametinga fainali hiyo baada ya kuiengua Sahare All Stars iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa kuichapa bao 1-0, wakati Simba iliifunga Yanga kwa mabao 4-1.

Mechi hiyo imepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Nelson Mandela,uliopo Sumbawanga mkoani Rukwa na utachezeshwa na waamuzi sita.

Mbali na kutwaa ubingwa, Lusajo alisema kuwa ndoto yake ni kufumania nyavu katika mchezo huo ili aingie katika vitabu vya kihistoria.

"Ukiachana na ubingwa ninaotamani, pia nataka kuacha rekodi ya kufunga bao, kama nilivyofanya ligi kuu nina mabao 12 yakukumbukwa,"amesema Lusajo.