JAMANI NINI KIMEMKUTA SHAABAN CHILUNDA?

Tuesday July 7 2020

 

Ni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC dhidi ya Singida United katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.

Dakika ya 63, kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba anamtoa Richard Djodi na kumuingiza Shaaban Idd Chilunda.

Chilunda, zao la akademi ya Azam FC usoni anaonekana amechoka na asiyejiamini. Mwili unaonekana mlegevu na ulioongezeka uzito. Anajikongoja kuingia uwanjani. Anagusa mpira wa kwanza, wa pili, wa tatu...tayari yuko taabani.

Hawezi tena kuufurahia uwanja. Hawezi tena kukimbia na mpira. Hawezi tena kutoa pasi ya uhakika na hawezi tena kufunga.

Chilunda huyu ni tofauti kabisa na Chilunda wa Taifa Stars ya CHAN, aliyeingia dakika ya 63 dhidi Sudan mjini Omdurman, Oktoba 18, 2019, na kutengeneza bao la ushindi lililoifanya Tanzania ifuzu CHAN 2020.

HUYU WA SASA

Advertisement

Dakika zake 27 uwanjani dhidi ya Singida United, alizitumia kuwakera watazamaji na hasa mashabiki wa Azam FC, bila shaka hata mabosi wake, na zaidi kocha wake.

Alipata mpira ndani ya 18 upande wa kulia, akiwa mbele ya beki wa Singida United, akaingia ndani ya sita. Lakini pumzi ikakata akashindwa kupiga ili afunge.

Akapunguza kasi hadi yule beki akafika. Akajaribu kumpiga chenga lakini akaanguka mwenyewe na beki akachukua mpira...shambulizi limekufa.

Akapata tena mpira upande wa kushoto nje kidogo ya 18. Kulia kwake yupo Obrey Chirwa akiwa peke yake...badala ya kumpasia, akaamua kuingia nao ndani ya 18 akifukuzana na beki, yeye akiwa mbele. Akajitangulizia ndefu, lakini akashindwa kufika kwenye mpira, akaanguka na kupoteza umiliki. Shambulizi limekufa.

Akapata tena mpira nje kidogo ya 18 upande wa kulia, kushoto kwake yuko Idd Nado.

Safari hii akajaribu kumpasia Nado, lakini mpira ukamgonga beki wa Singida United ambaye hakuwa tishio kabisa kwa hilo shambulizi, mpira ukapotea, shambulizi limekufa.

YULE WA SUDAN

Dakika zake 27 alizitumia kuwafurahisha watanzania waliokuwa wakiufuatilia mchezo huu kupitia luninga.

Huo ni wakati wa msemo wa UPEPO WA KISULISULI (RIP Mama Rwakatare), ambao mtangazaji Baraka Mpenja aliutumia pale Stars walipofunga mabao yao.

Dakika ya 78, Chilunda aliukimbilia mpira ambao katika hali ya kawaida angeweza kuuacha na wala hakuna mtu ambaye angemlaumu. Mpira ule ulikuwa unaelekea kufa, lakini akaupa uhai...akamlamba chenga matata sana mlinzi mmoja wa Sudan na kupiga krosi iliyomaliziwa na Ditram Nchimbi.

Ukiwanagalia Chilunda hawa wawili, unaona ni watu tofauti kabisa, lakini kumbe ni kijana yule yule kutoka Tandahimba.

MASIKINI CHILUNDA

Hadi sasa ana mabao matano tu kwenye ligi tofauti na msimu wake wa kwanza wa 2016/17 ambao alicheza kuanzia dirisha dogo lakini alifunga mabao saba.

Ukimchukua Chilunda huyu na kumlinganisha na yule aliyefunga bao la tiktak dhidi ya Yanga utasikitika sana. Au yule aliyefunga mabao manne peke yake dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kwenye robo fainali ya Kombe la Kagame 2018, utamuonea huruma. Nini kimemkuta Chilunda?

Advertisement