Chilunda aitosa CD Tenerife, arudi Azam FC

Muktasari:

Azam imeshindwa kufikia makubaliano na CD Tenerife juu ya usajili wa moja kwa moja wa Chilunda na kumlazimu mshambuliaji huyo kurejea nchini.

Dar es Salaam.Ndoto nzuri ya Shaban Chilunda kucheza soka Ulaya imefikia mwisho baada ya klabu yake ya Azam FC kushindwa kufikia makubaliano na CD Tenerife ya mshambuliaji huyo kubaki kwa msimu kwa 19/20.

Chipukizi huyo wa Tanzania alijiunga na CD Tenerife msimu wa 2018/19 na kufanikiwa kucheza mechi tatu za ligi kabla ya kutolewa kwa mkopo kwa CD Izarra (ya daraja la pili B).

“CD Tenerife inachukua nafasi hii kumtakia Chilunda mafanikio mema ya maisha yake kisoka na binafsi,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.

Chilunda kwa sasa amerejea nchini akiwa katika kikosi cha Tanzania ‘Taifa Stars’ wakijianda na mashindano ya Afcon, Misri.

Mapema Mei 5, 2019, klabu za CD Tenerife na CD Izarra walikubalia baada ya nyota huyo kumaliza muda wa kucheza kwa mkopo Juni 30, wangewasiliana na klabu inayommiliki ya Azam FC ya Tanzania juu ya hatma yake.

Kwanza Chilunda alitakiwa kwenda Tenerife kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya chini ya jobo la madaktari wa CD Tenerife baada ya hapo ndipo mazungumzo ya kumchukua moja kwa moja yafanyike.

Uamuzi wa Azam kumrudisha Chilunda unafanana na ule waliofanya kwa mwaka 2014, baada ya Shomari Kapombe kugoma kurejea klabu yake ya Daraja la Nne Ufaransa, AS Cannes.