Tatizo kubwa la Chilunda hili hapa

Muktasari:

Baada ya mchezaji huyo kutua nchini siku za karibuni ameonekana akishiriki mazoezi na Timu ya Taifa jambo ambalo liliibua mjadala endapo ni salama kucheza huku akiwa na tatizo hilo.

NILIWAHI kuandika katika moja ya makala zangu siku za nyuma kuwa vilabu vya kulipwa bila kuwa na utimamu wa kiafya haviwezi kukusajili au kupata mkataba mpya wa kuvichezea.

Hii imedhihirika kwa mwanasoka kijana kutoka Tanzania, Shaaban Idd Chilunda ambaye mwaka jana alijiunga kwa mkopo klabu ya CD Tenerife ya Hispania inayoshiriki La Liga 2 akitokea Azam FC.

CD Tenerife nayo ilimtoa kwa mkopo kwa klabu ya CD Izarra ambao ulitarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu.

Chilunda amerudishwa nchini kwa kile kilichodaiwa kuvunjwa kwa mkataba baina yao, huku klabu hiyo ikieleza ana tatizo la kiafya lijulikanalo kitabibu kama Pericarditis.

Tatizo hili ni moja kati ya magonjwa ya moyo yanayojitokeza kwa uchache sana.

Baada ya mchezaji huyo kutua nchini siku za karibuni ameonekana akishiriki mazoezi na Timu ya Taifa jambo ambalo liliibua mjadala endapo ni salama kucheza huku akiwa na tatizo hilo.

Hata hivyo, mchezaji huyo amefichua tatizo lake hilo alishatibiwa ndio maana kwa sasa anaendelea kufanya mazoezi na kikosi cha Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kilichoondoka jana Alhamisi kwenda Misri.

Kwa kawaida klabu kubwa za kulipwa hufanya uchunguzi wa kina wa afya huku wakizingatia muongozo wa Shirikisho la Soka la duniani (FIFA) wa upimaji moyo kwa wachezaji pale wanapowasajili au kabla ya msimu kuanza.

Inaelezwa uchunguzi huo ndio uliobaini uwepo wa hitilafu hiyo ya moyo kwa mwanasoka huyo kinda.

Leo nitawapa ufahamu juu ya tatizo hili la kiafya ili kuwapa uelewa zaidi na kujua kama tatizo hilo la moyo linaweza kutuhatarisha wakati wa kushiriki michezo.

Pericarditis ni ugonjwa gani?

Pericarditis ni neno la sayansi ya tiba likimaanisha ni tatizo la kiafya linalotokana na uwepo au kujitokeza kwa shambulizi katika tando maalumu inayozunguka moyo ndani yake kukiwa na majimaji.

Kwa kawaida zipo tando mbili zinazouzunguka moyo ambazo huwa na nafasi inayokuwa na majimaji yenye kazi kama ya kilainishi. Tando hizi zimeubeba moyo kama vile mfano wa pochi iliyobeba kitu.

Pale panapotokea shambulizi katika tando hizo ndipo hutokea msuguano ambao husababisha kutokea kama dalili mbalimbali za ugonjwa huu.

Wanasayansi wa tiba hushindwa kubaini chanzo cha moja kwa moja kinachosababisha kutokea kwa tatizo hili katika moyo.

Lakini tatizo hili linahusishwa na vimelea vya virusi na shambulio la moyo (heart attack), vilevile matatizo mengine ikiwamo magonjwa yanayosababishwa na hitilafu ya kinga, VVU, kifua kikuu na baadhi ya dawa za matibabu.

Tatizo hili linaweza kuwa la muda mfupi au sugu pale linapodumu kwa zaidi ya miezi mitatu.

Dalili za tatizo hili huwa ni kupata maumivu makali ya kuchoma kifuani katika upande wa katikati kuelekea kushoto eneo ulipo moyo ambayo huzidi wakati wa kupumua, pumzi kukatika, kupata homa, kuhisi mchoko, tumbo na miguu kuvimba na kuwa na mapigo ya moyo yasiyotulia.

Kwa kawaida tatizo hili linaweza kupotea lenyewe bila matibabu ya dawa yoyote kwani kinga ya mwili inaweza kulitatua.

Dawa za tiba za kudhibiti shambulizi zinaweza kutolewa na mara chache sana tiba ya upasuaji inafanyika ili kuondoa tando iliyoathirika.

Kuna madhara kucheza soka?

Kama tulivyoona katika ufahamu wa jumla, tatizo hili linaonyesha linaweza kuwa la muda mfupi na kujitatua lenyewe au kupewa dawa za kutuliza shambulizi la tando hizo.

Na tatizo hili lingelikuwa ni la kudumu kwa Chilunda ni dhahiri isingekuwa uamuzi sahihi kuendelea kucheza soka, kwani kutokana na ugonwa huu kitendo cha kupumua kwa kasi kunaleta maumivu makali kifuani.

Machapisho mbalimbali ya utafiti yanaeleza bado hakuna uthibitisho wa mazoezi kuchochea kuongezeka au kusababisha tatizo hilo kujitokeza.

Ingawa sayansi ya utendaji wa mwili inaonyesha kucheza au kufanya kazi kunasababisha tando zilizoshambuliwa za moyo kusuguana hali ambayo ndiyo inayosababisha maumivu makali ya kifuani.

Miongozo mingi ya tiba ya kimataifa ya tatizo la Pericarditis kutoka katika taasisi za moyo duniani zinaelekeza mwanamichezo ataruhusiwa kushiriki baada tu ya kuthibitika kuwa amepona kabisa.

Na ataruhusiwa kucheza michezo isiyo na ushindani.

Ieleweke pia ni kawaida tatizo hilo kuweza kujirudia hata baada ya kupona.

Hivyo ni vyema Chilunda akashikamana na ushauri wa madaktari kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara pamoja na ushauri kama anataka kuendelea kusakata soka kwa raha zake.