This is Simba buana!

Sunday June 28 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN

KUSHNEI! Ndio kauli unayoweza kutumia mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Tanzania Prisons waliokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kumalizika kwa suluhu na Simba kubeba ubingwa wao wa tatu mfululizo na wa 21 katika ligi tangu 1965.

Matokeo hayo yameifanya vinara wa ligi Simba kufikisha pointi 79, ambazo hakuna timu yoyote inayoweza kuzifikia hata kama wakipoteza michezo yake yote sita iliyosalia kwa maana hiyo kuweza kuchukua ubingwa msimu huu na inakuwa mara ya tatu mfululizo.

Simba wametwaa ubingwa huo wa ligi kwa mara ya tatu mfululizo na inakuwa awamu ya 20, kutwaa taji hilo wakikusanya pointi 79, wakicheza mechi 31, wakishinda 25, wakitoka sare nne, wakifungwa mitatu, wakifunga mabao 69 na wao kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 16.

Katika mchezo wenyewe ambao ulikuwa na upinzani wa aina yake kuanzia mwanzo mpaka mwisho Simba walionekana kuanza na kikosi ambacho kilikosa wachezaji saba wa timu ya kwanza ambao ni Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Francis Kahata, Pascal Wawa ambao hawakucheza kabisa wakati John Bocco, Luis Jose, Cletous Chama waliingia kipindi cha pili.

Simba waliingia katika mchezo huo wakiwa na nidhamu kubwa ya kushambulia na kuzuia kwa kuanza na mfumo wa (4-3-3), ambao uliwawezesha kuonesha upinzani mkubwa katika eneo la kiungo ambalo ndio lilikuwa na ushindani wa kutosha baina ya timu zote mbili.

Katika eneo hilo la kiungo Simba walianza na Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga na Gerson Fraga wakati Prisons walikuwa na Ezekiel Mwashilindi, Jumanne Nkazi na Adilly Buha ambao walikuwa wakishindana kwa matumizi ya nguvu na akili kila walipokutana kuna muda walikuwa wakichezeana faulo.

Advertisement

Ukiondoa ushindani huo ulikuwa katika eneo la kiungo mbali ya Simba kufanya mabadiliko katika eneo la ulinzi waliocheza Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Haruna Shamte na Gadiel Michael walikuwa na nidhamu kubwa katika kuzuia washambuliaji wa Prison Jeremia Juma, Salumu Kimenya na Samson Mbangula.

Kama washambuliaji hao watatu wa Prisons Kimenya, Mbangula na Jeremia kama wangekuwa na umakini wangeweza kuifungia timu yao bao hata la kuongoza kwani kila mmoja alipata nafasi ya kufanya hivyo kwa maana ya walinzi wa Simba kuokoa au kushindwa kulenga lango la wapinzani.

Prisons nao waliingia na nidhamu kubwa haswa kwenye kuzuia kwani muda mwingi walionekana kuwa nyuma ya mpira si chini ya wachezaji saba jambo ambalo walifanikiwa kuwazuia washambuliaji wote wa Simba ambao walionekana kufanya mashambulizi mengi kuwa ya kawaida kuliko yale hatari.

Simba walianza katika safu ya ushambuliaji walianza na Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu, Hassani Dilunga na Miraji Athumani na baadae aliingia Chama, Bocco na Luis Jose ambao wote walionekana kukubali kukabwa na kuzuiliwa na safu ya ulinzi ya Prison ambayo ilikuwa chini wameki wa kati Vedastus Kunambi na Nurdin Chona ambao walikuwa katika kiwango bora.

 

Vikosi

Tanzania Prisons: Jeremia Kisubi, Michael Ismail, Benjamini Asukile, Vedastus Kunambi, Nurdin Chona, Jumanne Nkazi, Salum Kimenya, Ezekiel Mwashilindi, Samson Mbangula, Jeremia Juma na Adilly Buha.

 

Simba : Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Gerson Fraga, Hassani Dilunga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Miraji Athumani.

Advertisement