Gwambina yachukua nafasi ligi kuu mapema Singida yaaga

Mashabiki wa Gwambina FC wakishangilia baada ya timu yao kupanda Ligi Kuu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba

Muktasari:

  • Gwambina rasmi imejihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao kutokana na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba, huku ikiandika rekodi ya kufanya hivyo kabla ya Ligi kumalizika.

WAKATI Singida United ikishuka rasmi leo Jumamosi baada ya kupokea kichapo cha bao 3-2 dhidi ya Lipuli FC, Gwambina FC yenyewe imepanda rasmi kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Bao la dakika za nyongeza lililofungwa na Meshack Abraham limeifanya Gwambina FC kutangaza kupanda Ligi Kuu msimu ujao baada ya kuilaza Pamba bao 1-0, mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Singida sasa itamalizia mechi zake sita zilizobaki ili kukamilisha ratiba ambapo itakwenda kujiandaa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkali kwa kila timu, Gwambina ilisubiri hadi dakika hizo kupata uhakika wa kuungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga kwa kufikisha pointi 44, huku ikiwa na michezo miwili mkononi.

Abraham amesema haikuwa rahisi kupanda Ligi Kuu kwani walianza safari hiyo tangu mechi iliyopita lakini wanashukuru leo kuandika historia ya kupandisha timu.

Ameongeza kuwa kilichowafanya kupanda Ligi kabla ya mashindano kumalizika ni ushirikiano wa timu lakini kujituma kwa wachezaji na kwamba wamefanya walichoahidi.

"Haikuwa kazi nyepesi kwa sababu tuliisaka sana nafasi hii muda mrefu na leo Mungu amesaidia tumefikia tulichohitaji, ushirikiano na kujituma kwa wachezaji na timu kwa ujumla ndio siri yetu" amesema mfungaji huyo pekee aliyewezesha Gwambina kupanda Ligi Kuu.

Hata hivyo haikuwa rahisi kwa timu hiyo ya wilayani Misungwi mkoani hapa kupata nafasi hiyo, kwani kabla ya mchezo huo Pamba ilisaka nafasi hiyo katika mchezo uliopita dhidi ya Transit Camp ambao uliisha sare ya bao 1-1.

Hata hivyo hatua ya Gwambina kupanda Ligi Kuu, iliamsha shangwe kwa mashabiki wake ambao walikuwa wamejitokeza kusapoti Chama lao katika safari hiyo ya matumaini.

Baada ya mchezo huo Pamba itapaswa kupambana katika michezo miwili iliyobaki kuhakikisha inashinda ili kujinasua nafasi za chini ikiwamo kukwepa kushuka daraja kwani pointi 25 ilizonazo haziifanyi kutamba kwa sasa.