Aussems ajipanga kusaka pointi tatu kwa Kagera Sugar

Muktasari:

Programu hiyo maalumu waliyopewa wachezaji wa Simba ilianza Jumamosi asubuhi baada ya nyota 15, waliokuwepo kupelekwa Gym ambazo zipo ndani ya viwanja vya Gymkhana, ambako wakipigishwa tizi la maana kama lile ambalo walikuwa wakifanya Afrika Kusini katika maandalizi ya msimu.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems akishtukia jambo na fasta kutengeneza programu itakayowaokoa katika mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Simba watakuwa wageni wa Kagera Alhamisi hii na Kocha Aussems katika kuhakikisha wanapindua meza baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo ndani ya misimu miwili dhidi ya wababe hao wa Kagera, ameandaa programu maalum kwa vijana wake.
Programu hiyo maalumu waliyopewa wachezaji wa Simba ilianza Jumamosi asubuhi baada ya nyota 15, waliokuwepo kupelekwa Gym ambazo zipo ndani ya viwanja vya Gymkhana, ambako wakipigishwa tizi la maana kama lile ambalo walikuwa wakifanya Afrika Kusini katika maandalizi ya msimu.
Mazoezi hayo ya Gym yalikuwa yakisimamiwa na kocha wa viungo Adel Zrane na katika kuhakikisha kila mchezaji anafanya vizuri, Aussems alikuwa akimfuatilia mmoja mmoja kuona anachofanya na alikuwa mkali kwa kila aliyeonekana kutegea au kushindwa kufanya kama vile ambavyo anataka.
Aussems alisema kushindwa kupata matokeo ya ushindi katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Kagera msimu uliopita, kulimfanya kwenda kuangalia udhaifu wao na ubora wa timu pinzani hadi wakawazidi.
“Niliangalia tena marudio hadi ile mechi ya msimu wa 2017-18 tuliyopoteza kwa kufungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Shida kubwa kwetu wachezaji kuna muda wanapoteza nguvu ya ushindani kwa maana ya kuwashindwa kuwapiga presha mwanzo mwisho wapinzani,” alisema Aussems.
“Ili tuweze kushambulia kwa nguvu kwa muda mwingi ni lazima kila mchezaji awe fiti kwa maana ya utimamu wa kimwili na katika kuhakikisha hilo linafanikiwa nimelazimika kubadili ratiba ya kuacha kufanya mazoezi ya uwanjani na tumefanya haya ya nguvu gym.
“Hata wale wachezaji waliokuwa katika kikosi cha Stars, hawatakuwa na muda wa mapumziko kama ilivyo kawaida kwani leo Jumatatu, wanatakiwa kuwepo kambini ila watafanya kwanza mazoezi mepesi peke yao pembeni lakini kabla ya kucheza dhidi ya Kagera nao lazima wapate hata awamu moja ya kufanya mazoezi ya nguvu ya gym,” alisema Aussems.
Aussems alisema shida nyingine ambayo aliiona katika mechi tatu dhidi ya Kagera ni wachezaji wake kujiamini kupita kiasi, jambo ambalo wataliepuka katika mechi inayofuata.
“Tumegundua pia tumekuwa tukikosa nafasi nyingi za kufunga kama msimu uliopita Emmanuel Okwi, na washambuliaji hawakuwa makini katika nafasi walizopata na hilo hata msimu huu katika michezo ya kimashindanmo tumekuwa nalo lakini katika mazoezi yetu ya siku tatu nalo tumelifanyia kazi ili kufanya vizuri na kuondoka na ushindi kama malengo yetu yalivyo,” alisema na kuongeza pia anawakomalia washambuliaji wake juu ya umakini wakipata nafasi.

NYOTA STARS WATIBUA 
Katika hatua nyingine kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kilikuwa na wachezaji wanane kutokea Simba ambao ni Gadiel Michael, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Haruna Shamte, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Miraji Athumani na Hassan Dilunga.
Kutokuwepo kwa wachezaji hao katika mazoezi ya wiki moja kutokana na kuwa katika majukumu ya kitaifa, Aussems alisema kuna mahali ambapo vitu vya kiufundi vitaathirika katika timu yake.
Aussems alisema kuitwa Stars kwa nyota hao wanane ni ishara kwamba wako katika viwango vyao bora klabuni ambako walikuwa wakitumika mara kwa mara na mazoezi waliyoyafanya wiki iliyopita ilipaswa nao wawepo lakini watalazimika kujipanga kivingine.