Shikhalo asimulia ushindani wake na Metacha, Kabwili Yanga

Muktasari:
Baada ya kuyumba katika eneo la golikipa Yanga, imewasajili makipa wawili Mkenya Farouk Shikhalo na mzawa Metacha Mnata wote wakiwa makipa namba mbili wa mataifa yao.
Dar es Salaam.Kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo amesema hana wasiwasi na ubora wake katika kuwania nafasi mbele ya kipa mwenzake Metacha Mnata.
Shikhalo amesema uwepo wa Metacha una maana kubwa ndani ya timu hiyo na ushindani wao wa nafasi utaisaidia timu yao na kiwango vyao.
Kipa huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea Bandari ya Kenya alisema kwa mechi ambazo Yanga inacheza kwa msimu mzima sio kitu rahisi kwa kipa mmoja kucheza zote peke yake na kwamba inahitaji kushirikiana.
Alisema juhudi zao kuanzia mazoezini hadi katika mechi ndiyo kigezo kikubwa ambacho kimewafanya kuendelea kuitwa katika timu za mataifa.
Mkenya huyo alisema ataendelea kupambana kuhakikisha anakuwa na ushawishi kwa makocha wake na wala hatakuwa na kinyongo nafasi hiyo akipewa kipa mwenzake.
Akizumzungumzia kipa chipukizi Ramadhan Kabwili alisema ni kipa mzuri kwa kuwa bado umri wake unamruhusu kuendelea kujifunza zaidi.
Tangu atue Yanga, Shikhalo amecheza mechi moja ya kimashindano ya Ligi Kuu Bara akiruhusu bao moja dhidi ya Ruvu Shooting huku Metacha akidaka mechi tatu za Ligi ya Mabingwa akiruhusu mabao mawili.
Hata hivyo Shikhalo hakuweza kukaa langonj katika mechi mbili za kwanza za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers ya Botswana kutokana na kuchelewa kwa kukamilika kwa usajili wake kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).