Tufail atwaa taji la mashindano ya mbio fupi ya Ling Long

Muktasari:

Tufail alitumia muda wa dakika 2.46 kumaliza wa kwanza kilometa 2.5 katika mashindani hayo yaliyoandaliwa na Chama Cha Mbio za magari Tanzania (AAT) na kudhaminiwa na kampuni ya Ling Long Tire kutoka China na Artan Limited ya Tanzania.

Dar es Salaam.  Dereva nyota Tanzania, Tufail Tufail ameshinda mashindano ya kwanza yam bio fupi za magari (motorsport sprint event) zilizofanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers, jijini.

Mbio hizozilizo julikana kwa jina la Ling Long tire sprint event, zilishirikisha jumla ya madareva 11 kutoka mikoa ya Iringa, Morogoro na Dar es Salaam.

Tufail alitumia muda wa dakika 2.46 kumaliza wa kwanza kilometa 2.5 katika mashindani hayo yaliyoandaliwa na Chama Cha Mbio za magari Tanzania (AAT) na kudhaminiwa na kampuni ya Ling Long Tire kutoka China na Artan Limited ya Tanzania.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na dereva maarufu wa mashindano hayo, Bob Taylor kutoka Morogoro ambaye alitumia muda wa dakika 2.48 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na dereva mkongwe, Kirit Pandya aliyetumia muda wa dakika 2.51.

Mzee Pandya pamoja na kuwa na umri mkubwa, aliweza ‘kumchapa’ mwanaye, Dharam Pandya aliyemaliza katika nafasi ya nne kwa kutumia dakika 2.56. Dharam wikiendi iliyopita alishinda mashindano ya Afrika kwa upande wa Tanzania kwa kuwashinda madareva 14.

“Nimefarijika sana na ushindi huu, umeongeza makombe katika kabati langu, nimeweza kurekebisha makosa na kuibuka wa kwanza katika mashindano haya,” alisema Tufail.

Afisa Mtendaji Mkuu wa AAT, Yusuf Ghor alisema kuwa mashindano hayo mbali ya kutafuta washindi, pia yatatumika kama sehemu ya kuutangaza utalii kupitia michezo.

“Tumepata wageni 100 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo, China, Misri, Falme za Kiarabu na nyinginezo kwa ajili ya kuona maendeleo ya mchezo huu kwa ujumla na kutembelea vivutio vya utalii,” alisema Ghor.

Mkurugenzi wa Masoko wa Ling Long ukanda wa Mashariki ya Mbali na Asia, Kevin Chang alisema kuwa amevutiwa na vipaji vya madareva ambao wameonyesha uwezo mkubwa kushindana.

Naye Mkurugenzi wa Artan Limited, Ismail Artan alisema kuwa wamefarijika kuona Tanzania ina vipaji vikubwa katika mbio za magari na kuahidi kuendelea kushirikiana na AAT ili kuendeleza mchezo huo.

Artan alisema kuwa kampuni yake inauza mataili na hivyo imeamua kuwa mdau wa kwanza kwani bila mataili, gari haiwezi kutembea na kushindana.