Solskjaer apigilia msumari wa Pogba

Muktasari:

Dirisha la usajili huko Ulaya bado lipo wazi hadi Septemba 2, lakini kocha wa Man United, Solskjaer amesisitiza kwamba kiungo wake huyo ana furaha kubwa ya kubaki Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer amemwaahidi Paul Pogba ataendelea kubaki Manchester United kwenye kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Kiungo huyo anayesakwa sana na Real Madrid, Pogba alisema kwamba bado kuna maswali mengi yanamtatiza kuhusiana na hatima yake huko kwenye kikosi cha Man United kama atabaki au kuondoka baada ya dirisha la usajili huu wa majira ya kiangazi huko Ulaya litakapofungwa.
Dirisha la usajili huko Ulaya bado lipo wazi hadi Septemba 2, lakini kocha wa Man United, Solskjaer amesisitiza kwamba kiungo wake huyo ana furaha kubwa ya kubaki Old Trafford.
Ole alisema:  “Wala sina wasiwasi kuhusu Paul. Asilimia 80 ya kila anachokisema kinaonyesha kwamba anafurahia muda wake anapokuwa hapa.”
Alipoulizwa moja kwa moja kama kiungo huyo mshindi wa Kombe la Dunia alilobeba akiwa na Ufaransa ataendelea kubaki kuwa mchezaji wa Man United hadi hapo dirisha la usajili wa Ulaya litakapofunga, Ole alisema: “Kwa upande wangu, ndio ataendelea kubaki.”
Pogba alitarajia kuanzishwa kwenye kikosi cha Man United kilichomenyana na Wolves huko Molineux usiku wa jana Jumatatu, ikiwa ni kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England wakipambana kushinda baada ya kuanza vyema kwa kuichapa Chelsea 4-0 uwanjani Old Trafford Jumapili iliyopita.
Pogba alitua Man United mwaka 2016 wakati aliposajiliwa kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo ya Pauni 89 milioni. Na taarifa zinasema kwamba mabosi wa Man United watashawishika tu kumuuza Pogba kama Real Madrid na timu nyingine inayomtaka, Juventus watatoa mara mbili ya dau ambalo wao walililipa, kitu ambacho kinawatesa Los Blancos kwa sasa, hawawezi kulipa Pauni 180 milioni kwa pamoja.