VIDEO: Huyu Shiboub wa Simba mbona atawafunga sana mjipange kweli

Monday August 19 2019

Huyu Shiboub, wa Simba Tanzania, Mwanaspoti, mbona atawafunga, mjipange kweli

 

By YOHANA CHALLE

Dar es Salaam. Kama kuna shabiki wa soka anaamini kiungo mpya wa Simba, Shiboub Sharaf amebahatisha tu kufunga mabao dhidi ya Azam, basi pole yake kwani mwenyewe amefunguka, mbona huo ni mwanzo tu na atafunga sana msimu huu.
Kiungo huyo alioyesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan, alifunga mabao mawili wakati Simba ikiitambia Azam kwa mabao 4-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam juzi Jumamosi, huku akitakata vyema kwenye pambano hilo.
Shiboub alifunga mabao yake yote kwa kichwa mbele ya mabeki wa Azam na kipa wao Razack Abalora na kuwafanya mashabiki wa Msimbazi kushindwa kujizuia kuliimba jina lake, kitu ambacho kimemjaza upepo kiungo mrefu, fundi wa mpira.
‘Shishi...Shiboboo...Shishi...Shibooo’ ni baadhi ya nyimbo zilizokuwa zikimbwa kutokana na mashabiki kukunwa na soka la Msudan, huku wale wenzao wa Yanga waliokuwa wachache uwanjani wakitania mtamchukia tu huyo...!
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Shiboub alisema kufunga kwake mabao hayo sio kama amebahatisha kwani ni kawaida yake kutupia kwani hata alipokuwa Sudan kazi hiyo amekuwa akiifanya na Wanasimba wajiandae kuhesabu mabao tu.
“Nimefurahi sana kufanikiwa kufunga, nitajitahidi kufunga kila ninapopata nafasi,” alisema Shiboub na kuongeza kuwa, siku zote anapokuwa na timu yoyote furaha yake ni kuona anaipa mafanikio na mashabiki wa Simba wajiandae kupata raha.
Alipoulizwa juu ya mchezo wao ujao wa marudiano dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, alisema hilo ni jukumu la kocha na kazi yake yeye ni kucheza kwa bidii kama atapewa nafasi.
Mabao hayo ya jana ni ya kwanza ya kimashindano kwa mchezaji huyo tangu ajiunge na Simba, lakini ni la tatu kwani alishafunga kwenye mchezo wa kirafiki wakati Simba ikiwa kambini Afrika Kusini, ilipovaana na Platnum Stars na kuilaza mabao 4-1.
Shiboub aling’ara kwenye mchezo huo wa juzi hasa baada ya kutoka kwa mshambuliaji John Bocco kwani alipata nafasi ya kutawala zaidi, akisaidia beki ya Simba zaidi kwenye hatari za mipira ya juu pamoja na safu ya ushambuliaji aliipiga tafu kama kawa huku Middie Kagere akionekana kufurahi kila mara na kupeana ishara ya tano na nyota huyo.
Msudani huyo ambaye yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Sudan ameanguka wino wa mwaka mmoja Msimbazi na alipata mafanikio makubwa na Al Hilal ambayo msimu uliopita ilimaliza Ligi Kuu nafasi ya pili huku Al- Merreikh SC ikitawazwa kuwa mabingwa.
Katika mchezo wa juzi baada ya kufanya yake kipindi cha kwanza, kipindi cha pili aliwasha moto kama kawa na kumpa wakati mgumu kipa wa Azam FC, Abalora pamoja na safu yake ya ulinzi baada ya kazi nzuri aliyokuwa akiifanya kabla ya kutoka dakika ya 84 kumpisha Mbrazil Gerson Fraga.
Mbali ya mabao ya Shiboub anayeivaa jezi yenye namba 8 iliyoachwa wazi na Haruna Niyonzima, mengine yaliwekwa kimiani na watokea benchi, Clatous Chama na Francis Kahata, huku ya Azam yakifungwa na Shaaban Chilunda na Frank Domayo.

Advertisement