VIDEO: Aussems atengeneza mfumo wa kuwabeba Ajibu, Kahata Simba

Muktasari:

Kutokana na hilo katika mifumo ambayo Aussems anaweza kutumia ni 4-3-3,-4-4-2, 4-2-3-1 na mingine ili apate matokeo mazuri zaidi.

SIMBA ipo hapa Afrika Kusini inajifua, lakini Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amegundua siri kubwa sana na kama itatiki, basi kikosi chake hakitafungwa kirahisi kwenye mechi zao na katika kudhihirisha hana hofu, amewapotezea kabisa watani wao Yanga.
Aussems aliliambia Mwanaspoti, amegundua unapokuwa na timu inacheza mfumo mmoja ni rahisi kufungwa pale wapinzani wako wanapogundua mbinu zako sasa msimu huu anaibuka na mambo mapya ili kuweza kuwabana wapinzani wao.
Alisema, katika msimu ujao anataka kikosi chake kitumie mifumo zaidi ya mitatu, tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambao hawakukuzidi mifumo miwili.
Zaidi ilikuwa 4-3-3 kwenye viwanja vizuri kama Dar es Salaam na anapobadilisha ni 4-4-2 zaidi kwenye viwanja vya mikoani.
“Kama nitafanikiwa katika hili, sifikirii kabisa kama kuna timu inaweza kutufunga. Wakati mwingine mnapokuwa na mbinu chache unampa adui nafasi ya kuwafunga lakini kama mna mbinu nyingi tofauti adui anapokuja hivi, mnaadilisha nyingine,” alisema Aussems aliyekifikisha kikosi chake robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Hiyo kitu wakati mwingine ndio ilikuwa ikitufelisha kwenye baadhi ya mechi, kwa kocha anayejua kusoma vizuri mchezo akiwajua kazi yake inakuwa kufanyia kazi kile mnachokifanya wakati wote na mnapokutana inakuwa changamoto.”
Alisema, katika kufanikisha hilo anahitaji kuwa na wachezaji ambao wanaendana na kile anachokitaka na sasa ndio anafanyia kazi kuona kama anaweza kufanikiwa.
“Nafikiri kwa aina ya wachezaji hawa naweza kufanikiwa hilo taratibu tutakuwa sawa, ngoja tuone. Msimu uliopita ilikuwa ngumu kufanya hivyo kwa sababu ya aina ya wachezaji niliokuwa nao,”  alifafanua.
Kutokana na hilo katika mifumo ambayo Aussems anaweza kutumia ni 4-3-3,-4-4-2, 4-2-3-1 na mingine ili apate matokeo mazuri zaidi.
Katika hatua nyingine, Aussems anajua Yanga wapo Morogoro wanajifua lakini amesema, hataki kusikia habari zao kwa sababu kazi yake ni kuinoa Simba ipate matokeo mazuri.
“Kwenye Ligi Kuu kuna timu nyingi tunapambana nazo, tunatakiwa kuzifunga zote na si kufikiria timu moja. Hata tukiwafunga hao tu na timu nyingine wakatufunga hatuwezi kukamilisha ndoto zetu za ubingwa,” alisema Aussems.
Pamoja na kukutana na changamoto hizo, Simba imemaliza wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara ambao Aussems anataka kuutetea, pia walitisha katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walitinga robo-fainali kabla ya kutolewa dhidi ya TP Mazembe ya DRC.