Aston Villa yamuongezea maujanja Ally Ng’anzi huko Marekani

Muktasari:

Katika mchezo huo, Ng’anzi alicheza kwa dakika 20 tu baada ya kuingia dakika 70 akitokea benchi, lakini aliweza kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

KIUNGO Ally Ng’anzi anayekipiga katika Klabu ya Minessota United inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS), alipata nafasi ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Aston Villa akiwa na kikosi chake
Ng’anzi alirejea kwa mkopo akitokea Forward Mansion, lakini alijumuishwa katika kikosi cha Minessota ikiwa sehemu ya maandalizi ya msimu ujao
Katika mchezo huo, Ng’anzi alicheza kwa dakika 20 tu baada ya kuingia dakika 70 akitokea benchi, lakini aliweza kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.
Ng’azi aliliambia Mwanaspoti sehemu tu ya mchezo huo kumemfanya apate kitu kingine kikubwa ambacho kinamuongezea uzoefu katika maisha yake ya mpira.
“Nilichojifunza katika mchezo huo ni kujiongezea uzoefu, naweza kusema ulikuwa ni wa kawaida kwasababu tayari nipo huku kwa muda mrefu na nimeshazoea,” alisema.
Kocha wa timu hiyo, Adrian Heath, alisema ana uhakika Ng’anzi amefanya vitu viwili ambavyo wengine hawajafanya, anadhani akijituma atakuwa mchezaji mzuri baadaye.
“Amefanya vizuri na hata alipokuwa anapata mpira alikuwa akionyesha ni nafasi muhimu ameipata katika mchezo ule, alikuwa anataka kuonyesha vitu vya tofauti,” alisema.
Ng’anzi alikuwa katika kikosi cha Serengeti Boys kilichocheza fainali za vijana Gabon na  aliporejea alisajiliwa na Singida United, baada ya hapo aliondoka nchini na kujiunga na Klabu ya Czech, Vykov lakini hakukaa kwa muda mrefu na kutolewa kwa mkopo Minessota FC (Ligi Kuu Marekani) ambayo nayo ilimtoa kwa mkopo kwenda Forward Madison (Ligi Daraja la kwanza Marekani) na hivi sasa amerejea katika kikosi chake cha Minessota.