Zidane amtolea uvivu Bale amtaka aondoke Real Madrid

Muktasari:

Kisha baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ambayo walianza kwa majanga kama waliyomaliza nayo msimu uliopita kwa kupigwa 3-1, Zizzou akamalizia hasira zake kwa Bale.

TEXAS, MAREKANI. UKISIKIA bifu kali basi ndiyo hili. Zinedine Zidane hataki tena kuficha kwamba hamkubali kabisa Gareth Bale baada ya kubainisha kwamba anatamani winga huyo aondoke Real Madrid hata kesho.
Ishu ilianza hivi. Kwanza Bale hakuwamo kabisa katika kikosi cha Zidane kilichopangwa kucheza mechi yao ya kwanza ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Bayern Munich huko mjini Houston, Marekani juzi.
Kisha baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ambayo walianza kwa majanga kama waliyomaliza nayo msimu uliopita kwa kupigwa 3-1, Zizzou akamalizia hasira zake kwa Bale.
Alipoulizwa katika mkutano na wanahabari sababu ya kumuacha staa huyo nje ya kikosi, Zizzou alifunguka: "Bale aliachwa nje kwa sababu klabu inajaribu kumuuza.
"Kama akiondoka kesho, itakuwa bora zaidi.”
Kisha Zizzou akajiosha: “Hamna chuki binafsi, sina bifu lolote na Bale, lakini ni lazima nifanye uamuzi. Huwa kuna muda unafika unapaswa kufanya mabadiliko na ni jambo jema kila mtu akashika njia yake.
"Kuondoka ni uamuzi wa kocha, na pia mchezaji, ambao ndio wanaoujua ukweli wa mambo.
"Ukiangalia viwango vya baadhi ya wachezaji wapya walioitumikia Madrid kwa mara ya kwanza leo, hasa kinda Mjapani Takefusa Kubo, pamoja na kiwango cha timu kwa ujumla.
"Ilikuwa ni mechi yake ya kwanza Kubo," Zidane alisema.
"Hatujafurahishwa na kipigo, hakika tulitaka kushinda, lakini jambo muhimu lilikuwa ni kucheza tu kwanza hii mechi yetu ya kwanza rasmi.
"Kuna mambo chanya. Tulianza vyema, kisha tukaibadili timu yote kipindi cha pili. Tukawekwa kwenye presha.
"Lakini ndiyo kwanza hizi ni mechi za kujiandaa na msimu, na katika mechi ya pili kutakuwa na mabadiliko mengi. Kwangu, jambo muhimu zaidi si nani ameanza mechi."
Katika mkutano huo na wanahabari, kiungo wa Bayern, Thiago Alcantara aliweka wazi timu yao inamkaribisha kikosini Bale kama dili linaloripotiwa la kujiunga na miamba hao wa Ujerumani litatimia.
Bayern iinasaka mawinga wa kuziba mapengo yaliyoachwa na magwiji Arjen Robben na Franck Ribery walioondoka baada ya kumaliza mikataba yao.