Beki mkongoman atajwa Azam FC

Muktasari:
- Azam imeanza maandalizi mapema ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26, ikiwatambulisha baadhi ya wachezaji wake akiwemo kipa Aishi Manula, Muhsin Malima, Lameck Lawi na Kocha Florent Ibenge.
AZAM FC imeanza mazungumzo na Al Hilal ya Sudan ili kupata saini ya beki wa kulia, mkongomani Steven Ebuela, ambaye yuko nchini kwa takriban wiki sasa.
Azam imeanza maandalizi mapema ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26, ikiwatambulisha baadhi ya wachezaji wake akiwemo kipa Aishi Manula, Muhsin Malima, Lameck Lawi na Kocha Florent Ibenge.
Sasa taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni timu hiyo imeanza mazungumzo na Al Hilal ili kumnunua beki wa kulia, Ebuela.
Nyota huyo bado ana mkataba na mabingwa hao wa Sudan hadi Juni 30, 2027, alijiunga nao mwaka 2023 akitokea AS Maniema ya nchini kwao Congo.
Majibu waliopewa viongozi wa Azam baada ya mazungumzo ya awali ni ili kumwachia mlinzi huyo, wanapaswa kutoa zaidi ya Sh300 milioni.
"Ni chaguo la Kocha Ibenge, amependekeza kuongezewa beki huyo ambaye aliwahi kufanya naye kazi. Sasa mazungumzo bado yanaendelea kwa sababu bado ni mchezaji wa Al Hilal," kilisema chanzo hicho.
Kama Ebuela atasaini Azam, atakwenda kwenye eneo la beki wa kulia ambalo kwa sasa linashikiliwa na nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda, ambaye amekuwa na msimu bora akifunga mabao sita Ligi Kuu.
Akiwa na Al Hilal, Ebuela alicheza mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika akianza ya makundi dhidi ya Yanga kwa dakika zote 90, kijumla kacheza dakika 720 kwenye mechi nane.