Johora bado yupo sana Mashujaa

Muktasari:
- Kipa huyo alipoteza nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo akizidiwa maujanja na Patrick Muntari aliyemaliza na clean sheet 12 akiachwa nyuma tano na kinara Moussa Camara aliyemaliza na 17.
UONGOZI wa Mashujaa umeendelea kumshikilia kipa wao Erick Johora baada ya kumwongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kusalia katika kikosi hicho.
Kipa huyo alipoteza nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo akizidiwa maujanja na Patrick Muntari aliyemaliza na clean sheet 12 akiachwa nyuma tano na kinara Moussa Camara aliyemaliza na 17.
Chanzo cha kuaminika kutoka Mashujaa kililiambia Mwanaspoti wamemalizana na kipa huyo kwa kumwongeza mkataba wa mwaka mmoja huku akiweka wazi wanatambua ubora wake licha ya kuzidiwa na Muntari.
"Hatuwezi kuwa na kipa mmoja, lazima kuwe na watatu, hivyo licha ya kuwa hana namba kikosi cha kwanza, lakini anastahili kuwa sehemu ya kikosi chetu, ikitokea Muntari kapata shida yeye anaweza kukaa langoni," alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
"Ubora wa Johora unajulikana, kukosa kwake nafasi amekutana na mshindani lakini haina maana hana uwezo, naamini msimu ujao atakuwa sehemu ya ushindani ili arudi kikosi cha kwanza kwa sababu tunachokitaka ni ubora langoni."
Mtoa taarifa huyo alisema wameanza kumalizana na nyota ambao bado wanawahitaji na walikuwa sehemu ya mapambano msimu ulioisha wakiipambania timu hiyo iwe na uhakika wa kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.
"Tukimalizana na nyota tuliokuwa nao msimu ulioisha tutaanza kutoa majina ya sajili mpya ambazo pia tunaendelea nazo kutokana na ripoti ya mwalimu inayotutaka kuongeza nguvu sehemu mbalimbali za kikosi."