Yanga Singida wamvisha ushujaa Zahera

Muktasari:

Tukio hilo limetokana na ufunguzi wa tawi rasmi la timu ya Yanga mjini hapa karibu na Uwanja wa Namfua.

Singida. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameshangazwa na upendo wa wana Yanga mjini Singida kwa heshima waliyompatia kumvisha ngao ya ushujaa.

Zahera ameonyeshwa kushangaa baada ya kuvishwa kimili na mkuki kama ishara ya kupambana kivita kwa kabila la Wanyaturu ambalo ndilo kubwa zaidi mkoani Singida.

Zahera amesema hajawahi kupokea vazi la aina hiyo nchini kwao DR Congo licha ya kubeba baadhi ya vikombe.

"Nawashukuru kwa hii mliyonipa kwani sijawapa chochote hata kwetu licha ya kutwaa makombe na timu ya taifa sijawahi kupewa kitu hiki asanteni sana," amesema Zahera.

Mjumbe kamati tendaji wa tawi la Yanga lililofunguliwa rasmi leo, Shaban Kisuda amesema sababu za kumzawadia vitu hivyo ni kumlinda na maadui.

Kisuda ameongoza kuwa silaha hizo za kijadi kuhakikisha anafanya vema zaidi kwa timu yao Yanga lakini pia kama kumbukumbu kwake atakaporejea kwao Kongo.

"Tumempatia zawadi kocha wetu Zahera ambazo ni kaniki na mkuki ambazo zote ni za jadi yetu wanyaturu kwa lengo la kumkinga na maadui lakini pia kuendeleza ubora wa timu yetu pamoja na ukumbusho kwake pindi atakaporejea kwao Kongo," alisema Kisuda.

Zahera atakiongoza kikosi chake kesho Jumatano dhidi ya wenyeji Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Namfua mjini hapa.