Simba Queens yaendeleza dozi, yanusa ubingwa WPL

Muktasari:

  • Msimu huu Simba imekomba pointi zote 12 kutoka kwa wapinzani wake Yanga na JKT, ikiifunga Yanga nyumbani na ugenini kisha kuchukua pointi tatu kwa JKT baada ya timu hiyo ya jeshi kutotokea uwanjani katika mechi ya mzunguko wa kwanza na kisha kupata ushindi katika mechi yao ya leo.

SIMBA Queens imeendeleza ubabe na kugawa dozi baada ya kuichapa JKT Queens mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ikiwa juzi tu imetoka kumchapa mtani wake Yanga Princess 3-1 na kusalia kileleni.Hadi kipindi cha kwanza kinaisha Simba ilikuwa inaongoza kwa bao moja lililofungwa na Aisha Mnunka katika dakika ya 5 akipokea pasi kutoka kwa Jentrix Shikangwa na kumfanya afikishe mabao 16 ikiwa ni tofauti ya bao moja dhidi ya kinara Stumai Abdallah mwenye 17 na kipindi cha pili ikaongeza lingine baada ya JKT kujifunga kwa mpira wa frii-kiki uliopigwa na Ruth Ingosi.Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kusalia nafasi ya kwanza na pointi 37 ikijiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa msimu huu bada ya kupishana pointi tisa na mpinzani wake JKT mwenye pointi 28. Simba inahitaji kushinda mechi mbili na sare moja kutwaa ubingwa wa tatu wa WPL ndani ya miaka minne.Msimu huu Simba imekomba pointi zote 12 kutoka kwa wapinzani wake Yanga na JKT, ikiifunga Yanga nyumbani na ugenini kisha kuchukua pointi tatu kwa JKT baada ya timu hiyo ya jeshi kutotokea uwanjani katika mechi ya mzunguko wa kwanza na kisha kupata ushindi katika mechi yao ya leo.Hadi mzunguko wa 13 Simba ndio timu ambayo haijapoteza mchezo wowote ikishinda michezo 12  na sare moja na imekuwa bora msimu huu ikianza kwa kuchukua ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuitoa JKT kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4.Huo utakuwa msimu bora kwa Simba kwani zilipokutana timu hizo msimu uliopita, JKT ilivuna pointi nne ikishinda mabao 2-1 ugenini na kutoa sare ya bao 1-1 nyumbani.MECHI ILIKUWA HAPA
Utamu wa mechi ulikuwa kwa viungo wa timu zote mbili, eneo ambalo lilivutia wengi kwani kulikuwa na kurupushani za hapa na pale.Hapa kulikuwa na vita ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Vivian Corazone ambaye hadi sasa ana mabao matatu dhidi ya Donisia Minja wa JKT ambao kiuhalisia aina yao ya uchezaji inafanana, wakipiga pasi za usahihi, lakini Corazone alionekana kuwa bora baada ya pasi hizo kufika kwa walengwa mara nyingi zaidi.Vita ya viungo wenye asili ya kukaba, Ritticia Nabbosa na Joyce Lema, ilikuwa na mvuto wa aina yake leo katika eneo hilo kwa kila mmoja akifanya yake, lakini Nabbosa alionekana kushinda bato nyingi akihakikisha eneo lake halipati madhara na kutowaruhusu mastraika wa JKT kupita eneo lake.WASIKIE WENYEWE
Baada ya filimbi ya mwisho, nahodha wa JKT Queens, Anastazia Katunzi alisema: "Mpira ni mchezo wa makosa, hatukuwa na presha, lakini wenzetu wametumia makosa tuliyofanya kutuadhibu, tunawapa pole mashabiki wetu na michezo iliyobaki tunaamini tutashinda."Beki wa Simba Queens, Violeth Nickolaus alisema: "Tulikuwa bora kuanzia kwenye kiwanja cha mazoezi ambako kocha alituelekeza kufanya na hivyo hatukuwa na presha mchezoni, tulifuata maelekezo ya walimu na tunashukuru tumepata pointi tatu."