JKT yavuta 20 milioni ikiizamisha Mtibwa

Muktasari:

  • JKT ndiyo ilianza kupata bao katika dakika ya sita kupitia kwa beki Edson Katanga aliyefunga kwa kichwa kabla ya Charles Ilamfya wa Mtibwa kusawazisha katika dakika ya 22 lakini JKT ikapata bao la ushindi katika dakika ya 90 kupitia kwa Sixtus Sabilo.

USHINDI wa mabao 2-1 ilioupata timu ya JKT Tanzania leo dhidi ya Mtibwa Sugar umewafanya mastaa wa timu hiyo kushinda bonasi ya Sh20 milioni kutoka kwa uongozi wa maafande hao huku ukiididimiza Mtibwa mkiani mwa msimamo.

JKT ndiyo ilianza kupata bao katika dakika ya sita kupitia kwa beki Edson Katanga aliyefunga kwa kichwa kabla ya Charles Ilamfya wa Mtibwa kusawazisha katika dakika ya 22 lakini JKT ikapata bao la ushindi katika dakika ya 90 kupitia kwa Sixtus Sabilo.

JKT na Mtibwa zimekutana katika mechi ya duru ya pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam zote zikiwa katika nafasi hatari kushuka daraja lakini ushindi huo umeifanya JKT kutoka kwenye mstari mwekundu kwa kufikisha alama 26 baada ya mechi 24 na kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo huku Mtibwa ikisalia mkiani na pointi 17 baada ya mechi 23.


Matokeo hayo yamekuwa ya kufurahisha kwa JKT ambayo ilikuwa haijapata ushindi wowote kwenye ligi tangu mwaka 2024 uanze lakini pia umewaingizia pesa wachezaji na benchi la ufundi kwani kabla ya hapo uongozi uliahidi kutoa Sh20 milioni kama watashinda.

Kocha msaidizi wa JKT, George Mketo amesema ni ushindi uliorejesha furaha na ari ya kupambana zaidi kwa timu katika mechi sita zilizosalia.

"Tumefurahi sana. Tulikuwa kwenye hatari ya kushuka daraja lakini tumetoka na sasa tunajipanga kuhakikisha tunabaki eneo salama. Naamini ushindi huu utarejesha utulivu katika timu na morali itaongezeka kwa wachezaji katika mechi zilizobaki," amesema Mketo.

Kwa upande wa kocha Zuberi Katwila wa Mtibwa amesema licha ya kupoteza mchezo lakini bado anaamini timu inaweza kufanya vizuri na kusalia kwenye ligi.

"Nikisema ndio mwisho wetu nitakuwa nawakatisha tamaa wachezaji na wanamtibwa wote. Nadhani bado kuna nafasi tunaenda kujipanga ili kufanya vyema kwenye mechi zijazo," amesema Katwila.