Zahera amchana Kakolanya kweupe unaambiwa

Muktasari:

Kabla ya mchezo wao wa leo Jumatatu na Tanzania Prisons uliopigwa jijini Mbeya, Yanga ilikuwa inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 35, katika msimamo wenye timu 20. Azam FC ni ya pili ina pointi 33, Simba ya tatu ina 27 na ya nne ni Mtibwa Sugar yenye 23.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema ameamua kuachana na kipa wake Beno Kakolanya kwa sababu hataki kupokea simu za viongozi wake.

Zahera amesema, alipewa taarifa hizo baada ya kuwasili akitokea Congo.

Zahera ambaye ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo amesema, baada ya kusikia kuwa Beno hataki kupokea simu na hawatafuti viongozi akawaambia waachane naye na atawatumia wachezaji wengine alionao.

"Sina taarifa na Kakolanya wapi anakwenda kwa sababu sijaongea naye zaidi ya kupewa taarifa hizo na viongozi wa timu,"alisema Zahera ambaye siku zote huwa hafichi mambo.

Zahera akaenda mbali na kueleza kuwa hakuwa na sababu ya kumtafuta na kumbembeleza kwa sababu kihalali, mchezaji ndiye anapaswa kumtafuta au kumpigia simu kocha wake.

"Nafikiri baada ya kipindi chote hicho kupita yeye ndiyo alitakiwa kunipigia simu na kunambia kinachoendelea lakini amekaa kimya, hata mimi siwezi kumtafuta wakati yeye hajafanya hivyo,"alifunguka Zahera ambaye kikosi chake kimecheza mechi 13, kati ya hizo ameshinda 11 na ametoa sare mbili.