Bocco apiga mbili Simba yatakata

Muktasari:

Simba inahitaji ushindi wa mabao mengi zaidi ili kujiweka katika mazingira mazuri katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Mbabane Jumanne ijayo.

Dar es Salaam. Mabao mawili ya mshambuliaji John Bocco yaifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ikicheza mbele ya mwekezaji za klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliyeoneka kwa mara ya kwanza Uwanja wa Taifa, ilipata bao la kwanza dakika 07 lililofungwa na Bocco akimalizia pasi ya Nicolaus Gyan.

Shangwe za mashabiki wa Simba ziliingia doa baada ya Guavena Nzambe kuifungia Mbabane Swallows bao la kusawazisha katika dakika 24, kwa shuti kali akiwa nje ya 18 na kumwacha kipa Aishi Manula asijue la kufanya.

Baada ya bao hilo Simba ilirudi mchezo na dakika 32, ilipata goli la pili lililofungwa na Bocco kwa mkwaju wa penalti baada kipa wa Mbabane Swallows kumchezea vibaya Emmanuel Okwi na mwamuzi kuamuru adhabu hiyo.

Pamoja na kuongoza Simba itajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi walizopata katika kipindi cha kwanza kupitia washambuliaji wake Okwi, Kagere kwa mashuti yao kushindwa kulenda lango.

Kikosi cha Simba: kipa Aish Manula, Nicolas Gyan, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.