Guede aiua Coastal Chamazi, safari ya ubingwa yashika kasi

Muktasari:

  • Guede anayefikisha jumla ya mabao manne ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, ameifanya Yanga kufikisha pointi 62, baada ya michezo 24, hivyo kuhitaji pointi 12 ili kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kijumla.


BAO pekee la mshambuliaji, Joseph Guede la dakika ya 76 limetosha kuipa Yanga pointi tatu muhimu dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Guede anayefikisha jumla ya mabao manne ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, ameifanya Yanga kufikisha pointi 62, baada ya michezo 24, hivyo kuhitaji pointi 12 ili kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kijumla.

Kadi nyekundu aliyopata beki wa Coastal Union, Lameck Lawi dakika ya 70 baada ya kumfanyia madhambi nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI ni ya 17 kutolewa tangu msimu huu umeanza.

Katika kadi hizo, Lawi anakuwa mchezaji wa pili wa Coastal Union kupewa msimu huu baada ya Haji Ugando aliyeonyeshwa wakati wa mchezo dhidi ya Simba Septemba 21, mwaka jana kwenye Uwanja wa Uhuru.

Yanga imeendeleza rekodi nzuri Ligi Kuu  mbele ya Coastal Union, kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga Machi 4, 2021, haijawahi kupoteza tena wala kutoka sare.

Mabao ya Coastal Union iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda yalifungwa na Erick Msagati na Mudathir Said huku lile la Yanga iliyokuwa inafundishwa na Kocha Mrundi, Cedric Kaze likifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Mkongomani, Tuisila Kisinda.

Tangu hapo Yanga ilipopoteza mchezo huo, imekutana na Coastal Union katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo imeshinda yote na kufunga jumla ya mabao 12 huku kwa upande wa Coastal ikiwa haijashinda wala kufunga bao lolote.

Mchezo wao wa kwanza kukutana msimu huu, Yanga ilishinda pia bao 1-0, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Clement Mzize dakika ya 71, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Novemba 8, mwaka jana.

Huu ni mchezo wa pili kwa timu hizi kukutana Aprili tangu mwaka 2011, katika Ligi Kuu Bara na mechi ya kwanza ilipigwa Aprili 8, 2015 na Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 8-0, ikiwa ni mechi iliyozalisha mabao mengi kwao tangu zilipoanza kukutana baina yao.

Katika michezo 24 Coastal Union iliyocheza msimu huu, imeshinda tisa, sare sita na kupoteza tisa ikiendelea kusalia nafasi ya nne na pointi 33.

Mchezo unaofuata wa Yanga itasafiri hadi Tabora kucheza na Mashujaa Mei 5, huku Coastal itaikaribisha Tanzania Prisons jijini Tanga.

MAKOCHA WAZUNGUMZA

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema lengo lao kubwa lilikuwa kupata pointi tatu jambo ambalo wamefanikiwa licha ya ugumu wa mchezo huo.

"Tumepambana kupata kile tulichokihitaji hivyo nashukuru kwa pointi hizi tatu hasa baada ya kuzikosa mechi iliyopita, hakuna mchezo mwepesi hivyo nawapongeza pia wapinzani wetu kwa kuonyesha ushindani."

Kwa upande wa Kocha wa Coastal Union Mkenya, David Ouma amesema kadi nyekundu waliyopata iliwaharibia malengo yao japo amesifu kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo.

"Mchezo ulibadilika baada ya kadi nyekundu kwa sababu uliona tulivyokuwa 11 kwa 11 ila nashukuru kwa jinsi walivyojitoa kwani sio rahisi kucheza pungufu kwa muda mrefu na timu kama Yanga yenye wachezaji bora."