Tanzania yapata mualiko michuano ya Karate Japan

Muktasari:

Haya ni mashindano ya 15 ya karate dunia tangu kuanzishwa kwake na Tanzania imewahi kushirikiki mara mbili katika mashindano hayo.

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Tanzania ya Mchezo wa Karate imepata mwaliko wa kwenda kushiriki katika mashindano ya Dunia ya Karate Japani Oktoba mwaka huu.

Mashindano hayo ya Karate ya Dunia huwa yanafanyika kila baada ya miaka mitatu na mwaka huu Tanzania imepata nafasi ya kipekee kwa kutoa jaji wa michuano hiyo (Sensei) Jerome Mhagama.

"Tanzania tumewaahi kushiriki mara mbili katika michuano hii, lakini hatukuwa tunapeleka timu, bali tulikuwa tunapeleka mchezaji mmoja mmoja.

“Tunaamini kuwa tunapeleka timu kama timu, kwani yale ya kwanza tulikuwa tunashindwa kupeleka timu nzima kutokana na sababu za kiuchumi, lakini hivi sasa tunajipanga mapema," alisema Mhagama

Aliongezea kwa kusema kuwa nafasi iliyopata Tanzania ya kushiriki michuano hiyo na kuingiza Jaji ni jambo kubwa sana na lakujivunia, kwani ni nafasi inayo liliwa na mataifa kibao.

Haya ni mashindano ya 15 ya Dunia tangu kuanzishwa kwake na Tanzania imewahi kushirikiki mara mbili katika mashindano hayo.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2011 mashindano hayo yaliyofanyika Thailand, Tanzania Ilipeleka mchezaji mmoja tu ambaye ni Mhagama na alifika katika hatua ya 16 Bora.

Mwaka 2014 Katika mashindano yaliyofanyika Japan, Tanzania Ilishiriki katika mashindano hayo kwa kupeleka Jaji, ambaye pia alikuwa ni Mhagama.