Ruto awaongoza Wakenya kushuhudia maajabu ya Kipchoge

Saturday October 12 2019

 

By Fadhili Athumani

MAKAMU wa Rais wa Kenya, Dk William Ruto, alikuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza Jijini Vienna, kumshuhudia Bingwa wa Dunia na mshikilizi wa rekodi ya Dunia ya mbio za Marathon, Eliud Kipchoge, akiushinda mkono wa muda.

Dk Ruto ambaye ni mpenzi mkubwa wa riadha, alionekana kwenye mstari wa watazamani wa kawaida, akifuatilia mbio hizo, ambazo zilimalizika kwa Kipchoge kuishangaza Dunia, alipoweka rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kumaliza Kilomita 42 ndani ya saa 1:59:40.

Mara baada ya mbio hizo kumalizika, ikiwa sekunde tisa mbele ya muda uliowekwa wa saa 1:59:49, Dk Ruto alikuwa wa kwanza kwenda kumpongeza Kipchoge, kabla ya Wakenya na mashabiki wengine kutoka kila kona ya Dunia kuungana naye.

Jana jioni kabla ya kufanyika mbio hizo maarufu kama INEOS 1:59 Challenge, ikienda na ujumbe wa ‘No Human is Limited’ kumaanisha hakuna binadamu anayeweza kushindwa jambo, Rais Uhuru Kenyatta, alimpigia Kipchoge simu, akimtakia kila la heri.

Akishindana na rekodi yake, Kipchonge alianza mbio hizo, taratibu kuanzia saa 3:15 asubuhi, kwa saa za Afrika mashariki (saa moja na dakika 15 kwa saa za Austria). Kwa kasi ile ile, kilomita 20 zilimalizika ndani ya dakika 57. Dunia inashangaa?

Hadi kufikia saa 4:44 asubuhi, tayari Kipchonge alikuwa amekamilisha kilomita 31, ambapo kwa mujibu wa mkono wa muda, zilimchukua saa 1:28:03 kumaliza kilomita na kubakisha kilomita 11 tu kuweka rekodi itakayotikisa Dunia. Alihitaji dakika 28 kujishangaa!

Saa tano kamili asubuhi, zilimkuta Kipchoge akimaliza kilomita 34, akiwa ametumia saa 1:40:34 na kubakisha kilomita sita, ambazo ni sawa na dakika 19, kuweka rekodi mpya. Kufika saa 5:10 tayari alikuwa amemaliza kilomita 39, akitumia muda wa 1:52:04 ambapo zilibaki kilomita 2.6 kukamilisha mbio.

Kukamilisha mbio hizo ndani ya muda huo maana yake nini? Maana ni kwamba, Kipchoge ndio mwanaume mwenye kasi zaidi duniani, kwenye mbio za Marathon, zimemuongezea Kipchoge Ksh 400 milioni ambazo ni sawa na Sh 8.9 bilioni kwa pesa ya Kitanzania kwenye akaunti yake.

Mbali na pesa hizo, Kampuni ya magari ya Isuzu, itamzawadi gari mpya aina ya Isuzu, Double Cabin, pia wadhamini wa mbio hizo, hawajasema ni kitu kitafuata baada ya ushindi huo. Historia imeandika na itabaki kukumbuka jina la Eliud Kipchoge!

Advertisement