Pogba anauzwa Pauni 83 milioni

Muktasari:

Wakala wake, Mino Raiola alisema wiki hii kwamba hakitakuwa kitu cha ajabu kama mteja wake huyo atarejea kwenye klabu yake ya zamani ya Juventus, ambayo aliitumikia kati ya mwaka 2012 na 2016.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United wameripotiwa kwamba wanajianda kumpiga bei Paul Pogba kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kwamba bei yake imeshuka hadi Pauni 83 milioni, mwenye pesa akiweka mezani mkwanja huo, anabeba.
Kiungo huyo Mfaransa ameshindwa kuitumikia timu yake msimu huu kutokana na kuwa majeruhi, akicheza mechi saba tu kwenye Ligi Kuu England na mwenyewe ameshasema kwamba anataka kwenda kukabiliana na changamoto mpya.
Klabu ambazo zimekuwa zikihusishwa na staa huyo ni Juventus na Real Madrid, lakini kwa mujibu wa The Guardian ni kwamba Man United haitakubali ofa ya chini ya Pauni 83 milioni.
Hata hivyo, bei hiyo itakuwa ya hasara kwa Man United, kwa sababu wao walitumia Pauni 89.3 milioni kunasa huduma yake walipomsajili kutoka Juventus mwaka 2016, lakini wakifikiria rekodi za majeruhi ya mara kwa mara anayopata kiungo huyo wanaona ni vyema kumpiga bei tu wachukue chao.
Wakala wake, Mino Raiola alisema wiki hii kwamba hakitakuwa kitu cha ajabu kama mteja wake huyo atarejea kwenye klabu yake ya zamani ya Juventus, ambayo aliitumikia kati ya mwaka 2012 na 2016.
Akizungumza baada ya Juventus kutoka sare ya 1-1 na AC Milan katika nusu fainali ya kwanza ya Coppa Italia, wakala Raiola alisema: "Italia panaonekana ni nyumbani kwa Paul. Hatakuwa na shinda kurudi tena Juve, lakini tusubiri tuone nini kitatokea baada ya michuano ya Euro. Paul anataka kucheza kwenye timu ya viwango, lakini hawezi kukimbiwa na Man United kwa sababu tu wapo kwenye hali mbaya."
Kocha Ole Gunnar Solskjaer alipanga Pogba awe kwenye mipango yake, lakini kwa hali ilivyo anaona sio kesi akiamwaachia tu aondoka. Staa huyo anatarajia kurejea uwanjani kwenye mchezo wa Manchester derby, Manchester United Machi 8.