Pep anasema Sterling atawafunga sana msimu huu

Muktasari:

Sterling alitarajia kuongoza Man City kwenye mchezo wa jana usiku walipotarajia kumenyana na Tottenham Hotspur huko Etihad kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, huku Guardiola akisema Spurs ni moja ya timu mbili bora za Ulaya kwa sasa.

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola anaamini staa wake Raheem Sterling atakuwa kwenye kiwango bora zaidi cha kutikisa nyavu msimu huu na kwamba atafikisha mabao 35. Msimu uliopita, staa huyo Mwingereza alifunga mabao 25 wakati Manchester City ilipobeba mataji yote matatu ya ndani huko England.
Ameanza kwa makali ya wembe msimu huu, akifunga kwenye Ngao ya Jamii na kisha akaja kufunga 'hat-trick kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England, wakati Man City ilipojipigia 5-0 West Ham United.
Alipoulizwa kama anadhani staa wake atafunga mabao 30 au 35 msimu huu, Guardiola alisema: “Ndio, ninamatumaini. Itakuwa nzuri kwake na kwa timu pia. Anapokuwa mbele ya goli, anaweka mpira kwenye nyavu.  Msimu uliopita alifunga 25 na 25 kwenda 30 ni mabao matano tu hapo.
“Anaweza kabisa. Anacheza vizuri, lakini tunahitaji zaidi na zaidi. Sijawahi kuzungumza na Sergio Aguero au Gabriel Jesus au Raheem, na yeyote yupo kwenye safu yetu ya ushambuliaji kuhusu ndoto na mipango yao. Akifunga nafurahi, siwezi kujali amefunga 30, 35 au 20.”
Sterling alitarajia kuongoza Man City kwenye mchezo wa jana usiku walipotarajia kumenyana na Tottenham Hotspur huko Etihad kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, huku Guardiola akisema Spurs ni moja ya timu mbili bora za Ulaya kwa sasa.
“Wao ni timu namba mbili bora kwa Ulaya kwa sasa. Hilo pekee yake linatosha. Tangu nilipokuja hapa, wamekuwa wakibadilika kila msimu na kuwa washindani, siku zote wamekuwa wagumu sana," alisema Guardiola akiwazungumzia Spurs kabla ya mechi yao ya usiku wa jana.