PAPY: Huyu anayetua sasa ndio mashine

NAHODHA na kiungo nyota wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kuwa, Mpiana Mozizi wa FC Lupopo ndiye aina ya straika halisi ambaye alikuwa akimtamani Yanga.

Tshishimbi ambaye huenda akasaini mkataba wa miaka miwili Yanga muda wowote kuanzia sasa, amesisitiza kwamba tangu atue Jangwani hajawahi kuona mchezaji mwenye ubora kama Mozizi pale mbele.

Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti, Tshishimbi alifichua simu aliyopigiwa na Mozizi na kuzungumza nae takribani dakika 17 akitaka kujua habari za Yanga na hali ya mambo ndani ya kikosi hicho.
Tshishimbi alisema Mpiana amemwambia ameshawishika kuja Yanga baada ya kuongea na mabosi wawili wa Yanga akiwamo mhandisi Hersi Said na kigogo mwingine ambaye yupo nje ya uongozi wa klabu hiyo lakini mwenye ushawishi mkubwa na sasa amekubali kutua Jangwani.
“Amenipigia juzi tu hapa nimeongea kwa muda wa kutosha tu ameniambia anataka kuja hapa Yanga na sio klabu nyingine sasa kuna mambo alitaka kujua kwanza juu ya timu yetu na nimemweleza amekubali ameniambia anakuja hapa Yanga,
“Mpiana ni mshambuliaji bora sana kama atakuja hapa nafikiri tangu niijue Yanga ndio watafurahi kuona kazi ya mshambuliaji halisi anayejua kupambana na kufunga ndio maana anaongoza kule Congo,” alisema akimzungumzia mchezaji huyo ambaye mpaka ligi ya Congo inasimama alikuwa na mabao 12, akifungana na Jackson Muleka wa TP Mazembe na Fiston Mayele wa AS Vita.

Tshishimbi alisema kwamba mchezaji huyo alimdokeza pia kwamba alishapata ofa ya Simba lakini sasa akili yake ameihamishia Yanga ambako anaona wako siriazi zaidi na rahisi kutoboa.

“Unajua nimekuwa nikiwashauri sana viongozi kuna wachezaji wazuri sana sehemu mbalimbali sasa kila nikiona kuna upungufu sehemu huwa nasema. Msimu huu na hata ule tulipata shida katika kufunga sana sasa tunahitaji watu bora kama alivyo Mpiana kule mbele tunatakiwa kuwa na nguvu naamini kwa viongozi ambao Mpiana amenitajia anawasiliana nao basi hakuna shaka watamleta akija watu wa Yanga watafurahi,” alisema Tshishimbi na kuongeza;

“Kule mbele tunahitaji hata watu watatu kusiwe na akili ya kumtegemea mtu mmoja au wawili kama kuna nguvu ya fedha basi walete hata Makambo na mwingine ili pale mbele kusiwe na kazi nyepesi. Tuangalie hata Simba msimu huu hata ule uliopita kule mbele walikuwa wana watu mpaka wanne wenye ubora mkubwa na wote wanafunga, ushindani unakuwepo, hakuna anayeweza kusumbua.

“Kazi hiyo sio kule mbele tu hata nafasi nyingine walete watu wa kweli wa kushindana ili ushindani uwe mkubwa na hiyo ndio timu kubwa kama Yanga,” alisisitiza Tshishimbi ambaye kila Alhamisi ana safu yake maalum ya ukurasa mzima kwenye gazeti hili akichambua soka.