Nchimbi: Wakati wa Mungu ni wakati sahihi

Muktasari:

Nchimbi alifunga goli la pili na ushindi katika mchezo dhidi ya Sudan uliomalizika 2-1.

STRAIKA Ditram Nchimbi aliyepeleka furaha kwa Watanzania baada ya kufunga bao la pili na ushindi katika mchezo dhidi ya Sudan jana Ijumaa usiku amesema hayo yote yametokana na uwezo wa Mungu.
Stars ilicheza mechi hiyo ya kufuzu fainali za CHAN na kushinda bao 2-1 huku wakiwa wamesonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyochezwa jijini Khartoum,  Nchimbi alisema kila kitu kina muda wake na yeye alikuwa anasubiri muda wake ufike ambapo Mungu amemuonyesha njia.
"Sikuwahi kukata tamaa ya kutokuwepo kikosi cha Stars, Mungu ameona sasa na siku zote wakati wa Mungu ni wakati sahihi leo nimeingia katika rekodi ya kuipeleka Tanzania CHAN," alisema.
Aliongeza kwa kusema "Nilikuwa nasema siku ambayo nitaitwa Stars nitaitumikia timu yangu kwa jasho mpaka tone la mwisho,"
Akizungumzia mchezo kiujumla alisema goli la kwanza walilofungwa katika mchezo huo lilitaka kuwatoa mchezoni lakini benchi la ufundi liliwatuliza.
"Pongezi ziende kwa benchi la ufundi kwani baada ya kwenda mapumziko tulirudi upya ambapo kocha alibadilisha mbinu, kwahiyo pongezi ziende upande wa benchi la ufundi," alisema.