Prime
Mambo matatu kuibeba Simba Morocco

Muktasari:
- Simba ambayo itaweka kambi ya siku kadhaa nchini Morocco kuanzia Jumatano hii, itakuwa pia na programu ya mazoezi ikilenga kuzoea hali ya hewa, aina ya nyasi na mbinu za kuzuia mashambulizi ya ghafla ya Berkane.
KOCHA wa Simba, Msauzi Fadlu Davids anaamini kuna mambo matatu muhimu ambayo yanaweza kuibeba Simba kwenye mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco Jumamosi hii.
Simba ambayo itaweka kambi ya siku kadhaa nchini Morocco kuanzia Jumatano hii, itakuwa pia na programu ya mazoezi ikilenga kuzoea hali ya hewa, aina ya nyasi na mbinu za kuzuia mashambulizi ya ghafla ya Berkane.
Simba inahitaji kuandika historia mpya historia ya ushindi wa kwanza nchini Morocco, historia ya kutwaa taji la kwanza la Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema miongoni mwa mambo mengine kuna vitu vitatu cha kwanza ikiwa ni uimara wa ukuta haswa pale kati kwa Abdulrazack Mohamed Hamza, Chamou Karaboue na Che Malone.
Pili, mastaa wote wamewaandaa kisaikolojia kupambana kupata matokeo ugenini na ndio maana wametaka kufika mapema zaidi.
Lakini, akasisitiza pia kuwa wachezaji wake katika siku za hivi karibuni wamezoea kucheza mechi ngumu za kufanya uamuzi.
Kocha Fadlu Davids anaamini kuwa licha ya timu yake kutokuwa na rekodi nzuri inapocheza Morocco, vijana wake wamejengwa kisaikolojia na wanaweza kuvuka changamoto hiyo kubwa.
“Ni mchezo mkubwa, lakini sisi tunakwenda kama timu iliyokomaa kisaikolojia na kimkakati,” alisema Fadlu.
“Tumejiandaa kuanzia nyuma hadi mbele, hasa ukuta wetu wa kati una nguvu kubwa. Hamza, Che (Malone) na Karaboue wameonyesha uimara na umoja ambao unatupa matumaini. Tunaheshimu rekodi, lakini hatuiogopi.”
Tangu Simba irudi kwenye ramani ya soka la kimataifa kwa nguvu, Morocco imekuwa ardhi ya maumivu kwao. Mwaka 2022 walikumbana na RS Berkane kwenye hatua ya makundi ya michuano hii, ikifungwa mabao 2-0 wakiwa Morocco, kabla ya kushinda 1-0 wakiwa nyumbani.
Hata hivyo, hii itakuwa mara yao ya pili tu kukutana na Berkane, lakini uzoefu dhidi ya timu za Morocco kwa ujumla unaonyesha ugumu mkubwa wa mechi za ugenini katika ardhi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Simba imeshakutana na vigogo wa Morocco kama Raja Casablanca na Wydad Casablanca. Katika rekodi ya mechi tisa dhidi ya timu za Morocco, Wekundu wa Msimbazi wameshinda tatu zote zikiwa ni mechi za nyumbani na kupoteza sita, bila sare hata moja ndani ya dakika 90.
Hakuwahi kushinda Morocco hata mara moja. Mwaka 2023 ilifungwa 3-1 na Raja Casablanca katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kufungwa 3-0 kwenye mechi ya kwanza Dar es Salaam.
Simba inajua fika kwamba mchuano huu hauhitaji siasa wala historia ya karatasi, bali nguvu, akili, na ustahimilivu wa kiushindani.
Hata hivyo, kwenye msimu huu wa Kombe la Shirikisho, Simba imeonyesha ukomavu wa hali ya juu ugenini. Katika mechi sita za ugenini msimu huu, Simba haijawahi kuruhusu zaidi ya mabao mawili. Ilianza kwa kutoa sare ya 0-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya kabla ya kuwafunga 3-1 nyumbani.
Katika hatua ya makundi, walipoteza mechi moja tu dhidi ya CS Constantine kwa mabao 2-1, ilitoa sare ya 1-1 dhidi ya Bravos do Maquis na kuwafunga CS Sfaxien kwa bao 1-0. Robo fainali ilifungwa 2-0 na Al Masry ya Misri lakini ikaja kupindua meza kwa ushindi wa penalti 4-1 baada ya kushinda 2-0 nyumbani.
Nusu fainali iliikabili Stellenbosch F.C. ya Afrika Kusini kwa kujilinda ipasavyo, ikishinda 1-0 nyumbani na kutoka suluhu ugenini mechi ambayo haikuwa na huduma ya Che Malone kutokana na majeraha.
Kurejea kwa Che Malone ambaye ameonekana kuwa fiti katika mechi ya Ligi dhidi ya KMC kunamletea ahueni Fadlu ambaye sasa ana chaguo la kuimarisha zaidi safu ya ulinzi. Katika mechi hiyo, Che Malone alicheza sambamba na Hamza na walionekana kuelewana vyema, jambo ambalo linatoa taswira ya ukuta madhubuti kuelekea fainali.
Mbali na hilo, Karaboue aliyesimama imara dhidi ya Stellenbosch anaongeza upana na ushindani wenye afya kwenye nafasi hiyo.
“Tunayo machaguo mengi sio katika eneo la beki kati tu, na hilo linatupa faida kubwa kimkakati,” alisema Davids.