Dube aendeleza moto, Yanga ikijikita kileleni

Muktasari:
- Ushindi huo ambao Yanga ilikuwa inacheza mechi yake ya 27 msimu huu, unakuwa wa 24 ikiendelea kujikita kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 73.
YANGA haijapoa, imeendelea kugawa vipigo ikiichapa Namungo ya Lindi mabao 3-0 huku majukwaani wakiendelea kupaza sauti kwamba 'Hatuchezi'.
Ushindi huo ambao Yanga ilikuwa inacheza mechi yake ya 27 msimu huu, unakuwa wa 24 ikiendelea kujikita kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 73.
DAKIKA 23 NGUMU
Dakika 23 za kwanza zilikuwa ngumu kuamini kama Namungo ingepoteza kwa idadi hiyo baada ya kuwabana vizuri Yanga na kufunga njia ya kukamilisha mashambulizi yao.
KOMBINESHENI YA AZIZ KI, NZENGELI
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 27 mfungaji akiwa kiungo Stephanie Aziz KI aliyepiga shuti kali akitoka kuanziana kona fupi na Maxi Nzengeli.
Wawili hao walianzisha kona hiyo kwa hesabu wakiwatoka Namungo na kwenda kufunga bao hilo safi lilifungua ushindi huo.
Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Azizi KI ambaye alikuwa Mfungaji Bora msimu uliopita na mchezaji Bora wa Ligi msimu uliopita huku Nzengeli ikiwa ni asisti yake ya tisa.
DUBE KAMA MZIZE
Wakati Namungo inajiuliza ikajikuta inaruhusu bao la pili dakika ya 31 mfungaji akiwa mshambuliaji Prince Dube kwa shuti dhaifu la mguu wa kushoto akigeuka kwa haraka na kumpoteza kipa wa Namungo, Jonathan Nahimana, mfungaji akipokea asisti ya beki wa kulia Kibwana Shomari ambaye alikuwa anatengeneza asisti yake ya pili msimu huu.
Bao hilo linakuwa la 13 msimu huu wa Dube akilingana na mwenzake Clement Mzize, wawili hao wanaendelea kumfukuza kinara wa ufungaji, kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua.
Alikuwa Nzengeli aliyemalizia idadi ya mabao kwa Yanga akifunga bao la tatu kwa mguu wa kushoto akimalizia krosi ya beki wa kulia, Israel Mwenda aliyeingia mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Kibwana.
HATUCHEZI
Kila Yanga ilipokuwa inafunga bao kwenye mchezo huo, mashabiki wake jukwaani walikuwa na wimbo mmoja tu wakiimba Hatuchezi ikiwa ni muendelezo wao wa kugomea mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba ambao uliahirishwa Machi 8, 2025 na kupangwa kuchezwa Juni 15, 2025.
ABUYA WAMOTO
Yanga itawapongeza wafungaji wa mabao hayo lakini pale kati kiungo Duke Abuya alikuwa ndio silaha nzito ambapo alifanya kazi kubwa akizima mashambulizi na kutawanya mipira.
NAMUNGO HALI MBAYA
Kipigo hicho ni taarifa mbaya kwa Namungo kwani kinazidi kuiweka kwenye wakati mgumu kuendelea kushuka chini kusogelea eneo la kucheza play off kupambani kubaki kwenye ligi kwani sasa ina pointi 31 kwenye nafasi ya kumi.