Mastaa Simba wampagawisha Sven

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck ameeleza maendeleo ya kikosi chake ni mazuri tangu walipoaanza kufanya mazoezi wiki moja iliyopita na kinatia raha.

Sven ameeleza maendeleo hayo ni utimamu wa kimwili kwa wachezaji wake, uwezo wao wa kupokea mbinu, ushindani wa kila mmoja katika zoezi ambalo anawapa na kiu ya kucheza.

Anasema yaani akiulizwa ataje wachezaji 11, ambao watacheza katika mechi husika ya kimashindano ni ngumu kwani kila mchezaji ameonesha kuwa na kiu hiyo katika mazoezi ya kikosi chao.

“Katika ufiti hatuwezi kufikia levo ile ambayo tulisimama nayo kabla ya ligi kusimamishwa na ile kufikia vile tunahitaji zaidi ya wiki sita za maandalizi,” alisema.

“Kikubwa ambacho nimekiona mpaka wakati huu katika kikosi changu ni ushindani ambao sikuwahi kuona tangu nimefika hapa jambo ambalo linaweza kunipa wakati mgumu pindi ninapochagua wachezaji 18.

“Naweza nikatoa nafasi kwa wachezaji fulani lakini wale ambao wapo benchi au hawakuvaa jezi kabisa ni kama nitakuwa nimewaonea kutokana na uwezo ambao wameonesha katika mazoezi wanastahili kucheza,” alisema.

“Hilo limechangiwa na wachezaji kuzifanyia kazi kweli programu ambazo tuliwapatia kipindi cha ligi kusimama lakini kila mmoja kuwa na kiu ya kutaka kucheza, kufanya vizuri kwa upande wake na timu kufikia malengo ambayo tulijipangia,” alisema Sven.