Makocha watambia vipaji U17

Wednesday July 10 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Makocha wa timu zilizofuzu nusu fainali ya mashindano ya vijana chini ya miaka 17 (Copa U17), kila mmoja ametamba kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Mechi za nusu fainali za mashindano hayo zitachezwa kesho Alhamisi kwenye Uwanja wa Chamazi ambapo Kinondoni itacheza na Kigoma wakati Morogoro itambana na Mwanza.
Katika nyakati tofauti, makocha wa timu hizo walijigamba kuwa bora ya mwenzake ambapo Kocha wa Kigoma, Hamis Mabo alisema, hana wasiwasi na vijana wake kwa sababu wamewaandaa kufanya vizuri na kufuzu fainali hizo.
Ahmad Simba ambaye ni Kocha wa Mwanza alisema, vipaji vya vijana wake na mbinu za soka ndivyo vitu anavyovitegemea katika mchezo wa kesho: "Najua ugumu wa mechi yetu, lakini  vijana wangu  wako vizuri, nimewaandaa kimchezo."
Kocha wa Kinondoni,  Evarist  Kitomongo alisema hana presha ya mechi, dakika 90 ndizo zitaamua matokeo kwani ana vipaji watakaompa matokeo kesho.
Naye Kocha wa Morogoro, Athuman Kairo alisema amewaandaa kiufundi na kisaikolojia vijana wake ambao anaamini watafuzu kucheza fainali kesho.

Advertisement