Lampard: Ziyech kiboko ya beki ngumu

Muktasari:

Akimzungumzia mchezaji wake huyo mpya, Lampard alisema: "Nafahamu ubora wake. Ni mchezaji ambaye tunaamini atakuja kuongeza ufundi kwenye timu.

LONDON, ENGLAND . KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard anaamini kwamba staa wake mpya aliyemnasa kwa Pauni 36.7 milioni, Hakim Ziyech ametua kwenye kikosi chake kwa kazi moja tu, kupangua ngome ngumu za wapinzani msimu ujao.
Ziyech, 26, atatua Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu baada ya klabu mbili, Chelsea na Ajax kufikia makubaliano ya kuuziana mchezaji huyo.
Akimzungumzia mchezaji wake huyo mpya, Lampard alisema: "Nafahamu ubora wake. Ni mchezaji ambaye tunaamini atakuja kuongeza ufundi kwenye timu.
"Alianza kunivutia baada ya kumtazama kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana, alikuwa mchezaji moto uwanjani hasa kwenye ile mechi dhidi ya Tottenham. Msimu huu tumekumbana naye mara mbili, hivyo nimepata fursa ya kumfahamu zaidi. Ana uwezo mkubwa wa kuutumia mguu wa kushoto, akiweza kucheza kwa kushambulia kupitia kulia na anaweza kutumika kama namba 10 pia.
"Ukituzama sisi msimu huu, kumekuwa na mechi nyingi ambazo tumekuwa tukipata shida kuzipenya ngome za timu pinzani, lakini kwa mchezaji huyo fundi naamini hilo litakuwa limekwisha.
"Tuna hakika atakuja kuleta kitu kingine tofauti kwenye timu. Nafahamu haji sasa, lakini klabu na mashabiki tunafurahi kwa taarifa hizo kwamba atakuwa wetu kuanzia msimu ujao."
Chelsea ilitoka kapa kwenye mechi dhidi ya Bournemouth, Southampton, West Ham na Newcastle msimu huu hivyo ilihitaji saini ya mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kupenya kwenye ngome ngumu ili kufunga mabao.